Serikali ya Sudan imemfukuza balozi wa Kenya nchini humo, kufuatia mahakama kuu ya Kenya kuamuru kukamatwa kwa Rais wa Sudan Omar al-Bashir, anayetafutwa na mahakama ya kimataifa ya ICC.

Balozi wa Kenya amepewa muda wa saa 72 awe ameondoka mjini Khartoum.

Jaji wa mahakama kuu ya Kenya Nicholas Ombija alisema mwanasheria mkuu wa serikali na waziri wa usalama wa ndani lazima watekeleze amri hiyo ya kumkamata iwapo Rais al-Bashir atakanyaga tena ardhi ya Kenya.

"lazima kuidhinishwe na Mwanasheria Mkuu na waziri wa mambo ya ndani iwapo rais Bashir atakanyaga Kenya", Jaji Ombija alisema.

Japokuwa Kenya ni mwanachama wa mahakama ya ICC, vyombo vyake vya usalama havikuweza kumkamata Rais al-Bashir wakati alipoitembelea Kenya mwezi Agosti, mwaka jana.

Baada ya tawi la shirika lisilo la kiserikali, tume ya kimataifa ya wanasheria (ICJ), iliomba mahakama kuu itoe hati ya kumkamata.

Wizara ya mambo ya nje ya Sudan awali ilijaribu kupuuza uamuzi wa jaji huyu ikisema uamuzi huo ulikuwa ni maswala ya ndani ya Kenya, ambayo hayange athiri uhusiano kati ya Sudan na Kenya.


kesi ya ICC

Bwana Bashir anasakwa na mahakama ya ICC kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari katika jimbo la Darfur.

Kenya imetia saini makubaliano ya kimataifa ambayo inamaanisha kuwa Kenya inaweza kutekeleza agizo la mahakama la kumkamata.

Sifa ya rais Bashir kimataifa ilififia zaidi baada ya mahakama ya ICC kutoa hati ya kumkamata.

Hata hivyo, tangu wakati huo Bashir ameungwa mkono na mataifa kadha ya kiarabu, ya Afrika pamoja na Uchina.