Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela(Kushoto).

Binti wa miaka 11 ambaye pia ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Mbezi Juu jijini Dar es Salaam, Media Agustino, amekutwa chumbani kwake akiwa amekufa baada ya kujinyonga.
Akithibitisha tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema mtoto huyo alikutwa chumbani kwake majira ya saa 5:00 asubuhi akiwa ameshakufa baada ya kujinyonga kwa kutumia kitenge chake ambacho alikitundika kwenye nondo ya dirisha.
Kamanda Kenyela alisema marehemu alichukua uamuzi huo baada ya kutokea ugomvi kati yake na kaka yake aitwaye Bonifasi Agustino (12), wakigombea kuwa ni nani atapika chakula cha mchana wa siku hiyo.
Alifafanua kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala na upelelezi unaendelea.

Wakati huo huo, mwanaume mmoja Ahmadi Mguhi (27), amekutwa chumbani kwake akiwa amekufa maeneo ya Mbagala Charambe Wilaya ya Temeke.
Kamanda wa Poilisi Mkoa wa Temeke, David Misime, alisema marehemu alikutwa chumbani kwake majira ya saa 1:30 asubuhi akiwa ameshakufa huku mwili wake ukiwa hauna jeraha lolote.
Alisema kuwa chanzo cha kifo hicho bado hakijafahamika kwani marehemu hakuacha ujumbe wowote kuhusiana na tukio hilo na hakukuwa na taarifa au dalili zozote za ugonjwa.
Mwili wa maerehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Temeke kwa uchunguzi zaidi na upelelezi unaendelea.