Waziri Mkuu wa Ugiriki anayeondoka madarakani George Papandreou


Viongozi wa Ugiriki wameafikiana kuunda serikali mpya ya muungano wa kitaifa, ofisi ya rais imesema.
Makubaliano hayo yaliafikiwa katika mazungumzo yaliyoongozwa na rais Karolos Papoulias mjini Athens, kati ya Waziri Mkuu, George Papandreou na kiongozi wa upinzani, Antonis Samaras.

Waziri Mkuu George Papandreou amekubali kujiuzulu na atakaye mrithi atachaguliwa katika mazungumzo yatakayofanyika Jumatatu, taarifa kutoka kwa ofisi ya rais ilisema.

Serikali hiyo mpya ya muungano ndiyo itakayoongoza nchi hadi uchaguzi mkuu ujao, ambao huenda ukafanyika 19 Februari, wizara ya fedha ilisema.

Tangazo la kuundwa kwa serikali mpya linajiri baada ya wiki moja ya mgogoro kuhusu madeni ya Ugiriki.


masharti ya EU
Muungano wa Ulaya umesema kuwa hautatoa mkopo zaidi kwa Ugiriki hadi pale mpango wake mpya wa kupunguzia nchi hiyo madeni utakapokubaliwa.


Kumekuwa na shinikizo kali kutoka kwa jamii ya kimataifa kwa Ugiriki kutatua mzozo wake wa kisiasa ili kuzuia kuyumbisha masoko katika muungano huo.

Punde kiongozi mpya atakapotaganzwa, rais Papoulius atazialika vyama vya kisiasa kujiunga na serikali hiyo.

Bwana Papandreou amekuwa akijaribu kuunda serikali ya muungano kurithi inayoongozwa na chama chake cha Pasok, lakini kiongozi wa upinzani Bwana Samaras wa chama cha New Democratic Party alikataa kushauriana naye hadi pale angejiuzulu.