MASTAA wawili, Irene Uwoya na Naseeb Abdul ‘Diamond’ wana mapenzi ya kichefuchefu, hawana misimamo kwa wapenzi wao, uhusiano wao unashilikiliwa na wazazi na si matakwa ya nyoyo zao.

Uwoya alishatangaza kumwagana na mumewe, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ kwa sababu hana mapenzi naye, lakini akarudiana naye kutokana na shinikizo la mama yake mzazi.

Vilevile, Diamond alishamuweka kando mchumba’ke, Wema Sepetu kwa madai lukuki, lakini mama yake mzazi, Sanura ‘Sandra’, aliposimama kidete, akarejesha mapenzi kwa Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006/07.

Wakati Uwoya anampa kibuti mumewe, mbali na maelezo kuwa hampendi, alisema pia kwamba Kataut ambaye ni mwanasoka wa kimataifa wa Rwanda si mwaminifu na ‘anamchiti’ kwa kidemu cha mtaa.

Diamond, yeye alidai kuwa Wema ni mvivu, hapiki, hafui, kazi zote za nyumbani alikuwa akifanyiwa na bi. Mkubwa (mama Diamond).


“Hata nguo zetu anafua mama,” Diamond alimtwanga dongo Wema.
‘Bwa mdogo’ huyo anayetusua hivi sasa kwa wimbo wake wa Moyo Wangu alidai pia kwamba Wema si mwema kwa sababu alikuwa anamlazimisha amfukuze nyumbani mama yake (Sandra).

Kutokana na matukio yao, yapo madongo wanayopigwa Diamond na Uwoya kuwa hawana nyoyo huru, mapenzi yao ni ya kulazimishwa.

Mcheza sinema mkubwa Bongo (jina tunalo), aliliambia Amani kuwa tabia waliyoonesha Diamond na Uwoya yanaashiria kitu cha hatari kwa Wema na Ndikumana siku za usoni.



“Ubaya wa Diamond na Uwoya wanaamua kwa mtindo mchafu, waliwaadhiri wapenzi wao kwa maneno mabaya kupita kiasi. Waliwafedhehesha mbele ya uso wa jamii.

“Uwoya kusema hajawahi kumpenda mume wake naye kuona hilo gazetini ni jambo baya kupita kiasi. Diamond kumsema Wema hapiki, hafui ni mambo hayapendezi ila ile sentensi kuwa alimshinikiza amfukuze mama yake ni balaa zaidi.

“Ile kauli inaweza kujenga chuki kwa mama yake, ingawa ndiye huyo aliyewafanya warudiane. Si ajabu kwa juu alisema warudiane lakini kwa ndani kuna kinyongo.

“Ndikumana na Wema ni watu wa kuonewa huruma, kwa maana kuwa na wapenzi wa aina hiyo, inaweza kuwagharimu mbele ya safari kwa sababu hawapo nao kwa matakwa yao, isipokuwa shinikizo la wazazi,” alisema staa huyo wa filamu akisisitiza jina lake lisitokee gazetini.

DIAMOND VIPI?
Staa huyo baada ya kurudiana na Wema alisema: “Nampenda Wema, ilikuwa tofauti na ikamalizwa na mama, ila ndani ya moyo wangu nampenda sana.”

WEMA JE?
Wema alisema: “Nilichogundua ni kwamba baby (Diamond) ananipenda, ilitokea mtafaruku umeisha. Mimi na Diamond tuna mapenzi ya kweli na penzi la kweli halifi.”

UWOYA NAYE!
Alipomaliza ugomvi na mume wake, Uwoya alisema: “Tuliachana kwa hasira, hata yale maneno kuwa simpendi Kataut ni kwa sababu ya hasira, nampenda sana mume wangu, tatizo huwa nina hasira za haraka.”

KATAUT
“Mimi sina tatizo, ni yeye ndiye aliyesema tuachane na sasa tumerudiana, namjua ana hasira za haraka. Ila siwezi kuchanganyikiwa, siwezi kujiua kwa sababu ya mwanamke hata ikitokea baadaye,” Kataut.