Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, amesema anatamani kutangulia ahera ili asione Tanzania ikiruhusu ndoa ya jinsia moja kama inavyoshinikizwa na Uingereza.
Dk. Mvungi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akitoa mada kwenye warsha ya kujenga uwezo wa ushiriki katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambayo iliwashirikisha wanaharakati na waandishi wa habari.
Alisema ni aibu kubwa kwa Tanzania ikiwa siku moja itaruhusu ndoa ya jinsia moja na kwamba ikiwa itafanya hivyo, itakuwa inakwenda kinyume na sheria za nchi kwa kuwa tendo la kulawiti ni kosa la jinai.
Alitaka Watanzania kupinga suala hilo kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha halipati nafasi na kwamba umaskini usiifanye Tanzania ipoteze heshima yake.
“Naomba Mungu siku ikitokea ushoga ukaruhusiwa mimi niwe nimekufa ili nisione kitakachokuwa kinaendelea,” alisema Dk. Mvungi ambaye pia ni mwanaharakati.

Alifafanua kuwa Uingereza inataka kuwaona Watanzania na Waafrika kwa ujumla ni wajinga na kuwashinikiza wakubali ndoa za aina hiyo wakati wao suala hilo hawajaliingiza kwenye Katiba yao.
"Jambo hili likiingizwa kwenye Katiba litapotosha taifa kwa kuwa lilianza kujipenyeza kwenye Kanisa la Anglikana lakini halikupata nafasi hivyo ni lazima lipingwe," alisema.
Juzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kitaifa, Bernard Membe, alitoa msimamo wa Tanzania kuhusu suala la ushoga ambapo alisema halikubaliki nchini.
Alisema wazo la Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon, kutaka nchi za dunia ya tatu zikubali suala la ushoga ndipo zipewe misaada halikubaliki na kwamba Tanzania ipo tayari kuikosa lakini ilinde heshima yake.