MCHEZA filamu mkali Bongo, Aunt Ezekiel ‘Gwantwa’ amekumbwa na tatizo kubwa ambapo akifanya kazi kwa muda mfupi anashikwa na usingizi mzito sana na ‘kuangusha gari’ popote, Amani limegundua.

Hivi karibuni, nyota huyo alinaswa na kamera ya paparazi wetu akiwa katikati ya usingizi mzito.
Ishu ilikuwa Mwananyamala Kwakopa, jijini Dar es Salaam ambapo msanii huyo na wenzake walikuwa wakirekodi filamu ya House Boy na House Girl kazi iliyoanza saa 10 alfajiri ya siku hiyo.

Aunt alishtuliwa na wasanii wenzake kwamba anapigwa picha na akaamka kwa tabu kama anayeumwa huku uso ukionekana kuchoka sana.

Msanii mwenzake, Kajala Masanja alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakicheza filamu hiyo, alimwambia mwandishi wa habari hii kwamba, Aunt alikuwa hajalala kwa siku tatu ndiyo maana alilala kama mfu.

“Unajua nini? Aunt hajalala usingizi kwa siku tatu, sasa hapo ulipomnasa ndiyo kama kapata nafasi ya kupumzika,” alisema Kajala.
Aunt mwenyewe alipoulizwa alijibu kwa shida:
“Kwa kweli hapa siwezi kuendelea na filamu bila kulala kidogo, najisikia vibaya sana.”
Hali iliyompata Aunt huwakumba watu wengi wanaokuwa bize bila kutenga muda wa kulala.
Kwa mujibu wa Daktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Godfrey Chale, tatizo la kufanya kazi mfululizo bila kutenga muda wa kupumzika husababisha ugonjwa ambao kitaalamu huitwa Hypoglycemia.

“Kwa kawaida ubongo unatumia asilimia 60 ya karoli za mwili, sasa mtu akiwa halali anasababisha ubongo ufanye kazi zaidi, kwa hiyo zilizopo zinakuwa hazitoshi.

“Hali hiyo husababisha hata ‘glukozi’ ipungue na kufanya mwili uwe na upungufu wa sukari, kwa maana mtu anapokuwa hapumziki hata ulaji wake unakuwa wa shida.”