BAADA ya misukosuko ya kuandamwa na skendo ya kesi ya rushwa, hatimaye mtangazaji mwenye jina kubwa Bongo, Jerry Cornel Muro amefunga ndoa ya kifahari jijini Dar es Salaam, Risasi Mchanganyiko linairusha hewani ‘laivu’ bila chenga.

Katika Ibada takatifu kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Azania Front jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita Jerry alikula kiapo cha ndoa alipofunga pingu za maisha na Jennifer John mwenye asili ya Uingereza.

JERRY MURO AKABIDHIWA RASMI JENNIFER
Kabla ya Ibada, baba wa ubatizo wa Jennifer aitwaye Renald Andreason, naye raia wa Uingereza, alimtoa binti huyo na kumkabidhi kwa Jerry mbele ya usharika wa kanisa hilo.

Baada ya Jennifer kutolewa mbele ya usharika, Mchungaji Anter Muro ambaye ni Mkuu wa Jimbo la Kaskazini, alifungisha ndoa hiyo iliyotawaliwa na vifijo na nderemo.

WAZUNGU WAFURIKA
Katika tukio hilo lililofurika raia wa kigeni (wazungu), lilichukua sura mpya wakati wa kuvishana pete ambapo kanisa hilo liligubikwa na nderemo na vifijo huku maharusi wakionesha tabasamu la furaha isiyo kifani.

KIAPO CHA NDOA
Jerry alikula kiapo: “Mimi Jerry Muro, nakubali Jennifer John awe mke wangu, katika shida na raha, katika dhiki na faraja, nimpende na kumtunza hadi kifo kitakapotutenganisha…”

Ilipofika zamu ya Jennifer, alifunguka: “Mimi Jennifer John, nakubali Jerry Muro awe mume wangu, katika shida na raha, katika dhiki na faraja, nimpende na kumtunza hadi kifo kitakapotutenganisha…”

SHEREHE
Ndoa hiyo ilifuatiwa na sherehe ‘babkubwa’ iliyofanyika katika Ukumbi wa Kramuu uliopo Mbezi Tangibovu, Dar ambapo watu walikula na kunywa hadi wakasaza.

Jerry aliwika alipokuwa akitangaza katika Kituo cha Runinga cha ITV na baadaye TBC1 kupitia kipindi cha Usiku wa Habari huku akiibua uozo wa polisi waliokuwa wakiomba na kupokea rushwa.

HUKUMU
Baadaye Jerry alijikuta nje ya fani akisota mtaani kutokana na kukabiliwa na kesi akidaiwa kuomba rushwa ili asitoe habari katika Kipindi cha Usiku wa Habari, hukumu yake itatolewa Novemba 30, mwaka huu.