BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars ‘Twanga Pepeta International’ itafanya onyesho kwa mara ya pili nchini Uingereza Jumamosi hii.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kampuni ya African Stars Entertainment
(ASET) inayomiliki bendi hiyo, Asha Baraka alisema wasanii 13 wanatarajiwa kwenda huko kwa
ajili ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru na Watanzania waishio Uingereza.

Baraka (pichani) alisema, wanamuziki wao wanatarajiwa kuondoka Ijumaa na onesho
litafanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa Silver Spoon, Wembley na kuwa bendi hiyo ikiwa huko itaendelea kufanya maonesho yake mengine kama kawaida nchini kwa vile baadhi ya wanamuziki watabaki.

Mara ya kwanza bendi hiyo kufanya onesho Uingereza ilikuwa mwaka 2007 ambapo ilifanya
maonesho matatu katika miji mbalimbali mikubwa duniani.

Wakati huohuo, Asha alisema anaingia mitaani kusaka wezi wa kazi za wasanii baada ya kugundua wizi kwenye CD zake za albamu mpya ya bendi hiyo.

“Twanga Pepeta ilizindua albamu yake ya 11 ya Dunia Daraja, albamu hii haijasambazwa kwa
mtu yeyote bado, tunaziuza wenyewe ukija kwenye maonesho yetu,” alisema na kuongeza kuwa wanashangaa kuzikuta kwa wafanyabiashara mitaani.