KOCHA Msaidizi wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema ari ya wachezaji wake iko juu kuelekea mchezo wa kwanza wa michuano ya Chalenji dhidi ya Rwanda Jumamosi ijayo.

Akizungumza na HABARI LEO jijini Dar es Salaam, Jamhuri ambaye ni msaidizi wa Charles Mkwasa kwenye timu hiyo, alisema ari ya vijana wake iko juu kiasi cha kumfanya aamini wataweza kutetea kombe hilo.

“Hata mimi mwenyewe imenishangaza, sikuamini wachezaji wana ari kubwa kiasi hiki, wakiendelea hivi wataweza kutetea kombe,” alisema Julio.

Aidha alisema wachezaji, Gaudence Mwaikimba na Haruna Moshi ambao walikuwa bado hawajajiunga na kambi ya timu hiyo, wamesharipoti na jana jioni kikosi hicho kilitarajiwa kuwa na wachezaji wote 28 mazoezini.

Akiuzungumzia mchezo wao huo dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi, kocha huyo alisema timu hiyo ni nzuri, lakini kwa jinsi anavyoona wachezaji wake wana nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

“Sio Rwanda tu, tunaweza kuifunga timu yoyote, vijana wamepania sana mashindano haya,” alisema Jamhuri.

Kilimanjaro Stars iko Kundi A na timu za Rwanda, Djibouti na wageni waalikwa katika mashindano ya mwaka huu timu ya Namibia.

Hata hivyo, aliwaomba mashabiki wa soka kuacha tabia ya kuzomea wachezaji wa timu hiyo, kwani kunawaondolea hali ya kujiamini.



Pia alitoa mwito kwa wadau na mashabiki wa soka nchini kuiunga mkono timu hiyo, kwani ni yao wote na si yake peke yake na kwamba ikifanya vibaya hataonekana yeye kama Julio kafanya vibaya bali ni taifa zima.

“Wasije wakakaa pembeni kwa kufikiri hii ni timu ya Julio, hapana ni yetu wote, tushirikiane,” alisema.