Kumekuwa na mlipuko wa kipindupindu katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani iliyopo Kenya, ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka Somalia wanaokimbia vita na ukame, umesema Umoja wa Mataifa (UN).

UN imesema ugonjwa huo huenda umetokana na wakimbizi wapya wanaowasili kambini hapo, ambapo mtu mmoja amekufa na sasa kuna taarifa za watu 60 kuwa na ugonjwa huo.

Shughuli za misaada katika kambi ya Daadab zilipungua mwezi uliopita kutokana na kutekwa nyara kwa wafanyakazi wawili.
Lawama
Kenya inatupia lawama kundi la wanamgambo la al-Shabaab kwa matukio ya utekaji nyara na imepeleka wanajeshi wake nchini Somalia kuwaandama wanamgabo hao.

Lakini al-Shabaab, ambayo inadhibiti sehemu kubwa ya kusini na kati mwa Somalia, inakanusha kuhusika na utekaji nyara.


Karibu watu nusu milioni wamekimbia Somalia na kutafuta misaada katika kambi ya Daadab katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema hali mbaya ya usalama bado inakwaza shughuli za misaada katika eneo hilo, licha ya polisi 100 kupelekwa huko mwezi uliopita.

Taabani


Shirika hilo limesema hali imezidi kuwa mbaya baada ya kipindupindu kuzuka. UNHCR na mashirika mengine yametenga maeneo maalum ya kutibu kipindupindu ndani ya kambi hiyo kwa watu walio taabani.

"Mvua na mafuriko yameathiri upelekaji wa maji katika maeneo ya kambi, na tunahofia kuwa baadhi ya wakimbizi waliamua kutumia maji ya mafuriko ambayo sio salama," imesema UNHCR, katika taarifa yake.

Ukame katika eneo la Afrika Mashariki ni mbaya kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka 60, huku Somalia ikiathirika zaidi.

Baadhi ya maeneo yametangazwa kuwa ya ukame mkubwa, na maelfu ya watu wamekimbia makazi yao kutafuta msaada nje ya mipaka.

Jeshi la Kenya kuingia nchini Somalia imechangia katika kupunguza idadi ya wakimbizi kutoka Somalia wanaoingia Daadab, lakini bado wengi wanakwenda Ethiopia.

Kambi ya tano ya wakimbizi inajengwa nchini Ethiopia na zaidi ya wakimbizi 7,600 waliowasili hivi karibuni kutoka Somalia kwa sasa wanahifadhiwa katika kambi ya muda, imesema UN.