Maelfu ya waandamanaji katika mji wa New York wameendelea na harakati zao wakielekea kuvuka daraja la Brooklyn, kuonyesha ghadhabu zao dhidi ya kuendelea kuwepo matabaka nchini humo.

Waandamanaji wanaadhimisha kuanza kwa kampeini ya kupinga mfumo wa kiuchumi unaosababisha matabaka nchini Marekani ambapo walipiga kambi katika mtaa wa Wall Street kuliko na soko kuu la hisa na taasisi kubwa za kifedha Marekani. Mwezi uliopita, polisi waliwakamata mamia ya waandamaji .

Taswira nje ya soko kuu la fedha la Marekani ni raia wenye ghathabu kubwa wakiendelea kukaribia jumba la soko hilo na kulizingira kabisa.Polisi wamekuwa na wakati mgumu kuwazuia kwa kuweka vizuizi nje ya jumba hilo. Baadhi ya waandamanaji wamekamatwa huku kukiwa na makabiliano na ujibizanaji wa maneno makali.

Hamasa ya waandamanaji hao ni kufuatia hatua ya polisi kuwafurusha katika eneo walikokita kambi katika bustani ya Zuccotti. Hii imewafanya kushindwa kukesha huko. umati wa watu ambao walikuwa wamekusanyika nje ya Wall Street wameondoka.

Hata hivyo wamepanga kukusanyika tena katika kituo cha treni na jioni watafanya jaribio jingine la kuvuka daraja kuu ya Brooklyne.

Waandamanji hao wanasisitiza kwamba ni haki yao kuandamana.