WATANZANIA zaidi ya 421 waliokuwa wakihitaji upasuaji mkubwa ukiwemo wa ubongo na uti wa mgongo na kutakiwa kutibiwa nje ya nchi, wamepatiwa matibabu nchini katika muda wa siku tatu na kundi la madaktari bingwa kutoka India.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni alisema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete kuhusu hali za wagonjwa hao.

Rais Kikwete alikwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukutana na madaktari hao mabingwa 16 pamoja na wataalamu wa afya wasiokuwa madaktari wawili kutoka hospitali za Madras Medical Mission Hospitali na hospitali za kundi la Apollo, ambalo limeanza maandalizi ya ujenzi wa hospitali kubwa na ya kisasa nchini.

Nyoni alisema mafanikio hayo matokeo ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya na tiba za magonjwa madogo na makubwa hapa nchini.

Nao wataalamu wa afya na madaktari hao wa ndani ya nchi na kutoka India, walimwambia Rais Kikwete kuwa kati ya wagonjwa hao zaidi ya 421, wagonjwa 12 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo na uti wa mgongo katika kipindi hicho na operesheni hizo zimefanikiwa.

Walisema kuwa wagonjwa wengine walipata huduma nyingine za tiba ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upasuaji mdogo na kuhudumiwa kutokana na magonjwa mbali mbali kama vile moyo, saratani ya ubongo, figo na nyonga.

Nyoni alisema wagonjwa hao wote ambao wamepata huduma ya afya na tiba katika kipindi hicho kifupi, tayari walikuwa wamekwishapata kibali cha wizara yake kwenda kutibiwa India na wengine walikuwa wanajiandaa kuondoka kufanyiwa uchunguzi nchini humo.



“Tumeokoa maisha ya wananchi na mamilioni ya fedha za umma kwa kufanikiwa kuwaleta mabingwa hawa kutoa huduma ya tiba hapa nchini, Mheshimiwa Rais.

“Hii ni kutokana na ukweli kuwa idadi hiyo yote ya wagonjwa walikuwa tayari wamepata vibali kutoka wizarani ama kwenda India kwa mara ya kwanza kutibiwa ama kurejea huko kwa mara nyingine ili kufanyiwa uchunguzi baada ya kuwa wametibiwa huko katika siku za nyuma,” alisema.