Marekani imefuta mchango wake wa fedha kwa Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, Unesco baada ya shirika hilo kuruhusu Palestina kuwa mwanachama kamili.
Uamuzi wa kuipa Palestina uanachama wa shirika hilo ulipitishwa na idadi kubwa ya wanachama licha ya upinzani mkubwa kutoka wajumbe wa Marekani na Israel.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani ametangaza kuwa malipo ya dola milioni 60 yaliyokuwa yatolewe mwezi ujao hayatatolewa na serikali hiyo.
Ada ya uanachama inayolipwa na Marekani ni moja ya tano ya bajeti ya mwaka ya Unesco.
Hili ni shirika la kwanza la Umoja wa Mataifa limeruhusu Palestina kujiunga nalo tangu utawala huo uwasilishe ombi lake la kutaka kutambuliwa kama taifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu.
Baraza la Usalama la Umoja huo litapiga kura mwezi ujao kuamua iwapo Palestina itaruhusiwa kuwa mwanachama.
Uamuzi wa Unesco kuikubalia Palestina uanachama umepongezwa na wengi kufuatia matokeo ya Jumatatu ambapo kati ya nchi 173 zilizoshiriki kupiga kura, 107 zilikubali, 14 zilipinga na 52 hazikupiga kura.
"Hii ni siku ya kihistoria," amesema naibu waziri wa Palestina wa mambo ya kale Hamdan Taha, akielezea suala hilo kila mahali huko Ramallah.

Uanachama katika Unesco unaweza kuonekana kuwa jambo geni na hatua moja kwa Wapalestina kupata taifa lao.
Lakini viongozi wanaona kuwa ni sehemu ya hatua kubwa ya kusukuma azma yao ya kutambuliwa kama taifa na kuishinikiza Israel.
Viongozi wakipalestina wanaiona kuwa hatua ya mwanzo ya ile muhimu zaidi mwezi ujao, wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakapoamua iwapo wapewe uanachama wa kudumu.
Marekani ina kura ya turufu katika Baraza hilo na imetishia kuitumia kupinga Palestina kuruhusiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Marekani haina nguvu hiyo katika Unesco na badala yake ilijaribu kushawishi nchi wanachama wengine kutoiunga mkono Palestina katika ombi lake.
Huenda kuwa Marekani itafuta michango yake kwa Unesco ipatayo dola milioni 70 kwa mwaka sawa na asilimia 22 ya bajeti yake ya mwaka.
Lakini wanachama wa Unesco wameonekana kutoa kipaumbele kwa masuala ya siasa badala ya fedha, wakiunga mkono ombi la Palestina.
"Huku ni kushindwa kwa Marekani" afisa mmoja wa Palestina alisema.
Matokeo haya yatamwongezea umaarufu Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas.
Rais Abba alipoteza jukwaa la kisiasa kwa wapinzani wake, Hamas wakati kikundi hicho cha kilipofanikisha kuachiliwa kwa mamia ya wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel walipobadilishana wafungwa hao na askari mmoja wa Israel Gilad Shalit aliyetekwa nyara kwa muda mrefu.
Nchi za Kiarabu zilikuwa msingi wa Palestina kushinda katika azma yake licha ya upinzani mkali kutoka kwa Marekani.
Katika kikao hicho, Uchina, Urusi, India, Brazil na Afrika Kusini zilipigia kura ombi la Palestina kuomba uanachama wa Unesco, huku Marekani, Canada na Ujerumani zikipinga na Uingereza haikupiga kura.