SHULE za msingi mkoani Morogoro zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati, hali inayowalazimu baadhi ya wanafunzi kutumia ndoo kama mbadala au kukaa sakafuni.

Upungufu huo umetajwa kuzikumba zaidi shule za vijijini ambazo baadhi hazina pia vyumba vya madarasa, hali ambayo wanafunzi wanalazimika kusomea chini ya miti na vibanda vilivyojengwa kwa miti.

Miongoni mwa shule za msingi ambazo gazeti hili limeshuhudia matatizo hayo, Lupiro iliyopo wilayani Ulanga, Mlandizi ya Wilaya ya Mvomero na shule ya Matongolo iliyopo Kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa.

Katika Shule ya Msingi Lupiro, chumba kimoja cha darasa la tano kinatumiwa na wanafunzi 179 ambao walishuhudiwa wengi wakiwa wamekalia ndoo na wengine sakafuni.

Shule ya Mlandizi Melela baadhi ya wanafunzi walikutwa katika mabanda na wengine wakiwa chini ya miti wakijisomea.

Licha ya shule za vijijini, kwa upande wa Manispaa ya Morogoro, taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera, Oktoba 23, mwaka huu inaonesha tatizo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, madawati yaliyopo kwenye shule zote ni 12,088 wakati mahitaji ni 29,132. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 38,266 mwaka 2005 hadi kufikia 45,699 mwaka jana ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 19.4.

Vile vile taarifa kuhusu Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, inaonesha ina mahitaji ya madawati 28,173. Yaliyopo ni 13,981 na upungufu ni 14,129. Kilosa ina mahitaji ya madawati 47,982 lakini yaliyopo ni 30,136.

Akizungumzia upungufu huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na Mvomero, alisema kuwa juhudi zimeanza kuchukuliwa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.

Bendera alisema katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha tatizo la upungufu wa madawati, nyumba za walimu na matundu ya vyoo linakuwa ni la kihistoria.