MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) pamoja na wanachama 11 wa chama hicho, wameswekwa mahabusu katika gereza la Kisongo lililopo nje kidogo ya jiji la Arusha.

Mbunge huyo na wenzie wamekumbana na mkono huo wa dola, baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali na kuhamasisha watu kukiuka sheria.

Lema na wanachama hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha, mbele ya Hakimu Judith Kamala.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Augustino Kombe aliieleza Mahakama kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walifanya makosa hayo Oktoba 28 mwaka huu.

Kombe alidai kuwa, makosa hayo ni njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu namba 384 na 385.

Kosa la pili kwa mujibu wa madai ya Kombe ni kufanya maandamano yasiyo halali ambayo yalianzia barabara ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, zilipo ofisi za mbunge huyo.



Kombe alidai kuwa maaandamano hayo yaliandaliwa, kinyume cha Sheria ya Polisi na kulikuwa na waandamanaji zaidi ya 100.

Katika kosa la tatu, Kombe alidai kuwa linamkabili Lema peke yake ambaye anashitakiwa kwa kuhamasisha watu kutenda kosa katika eneo la Clock Tower.

Kombe katika kosa hilo alidai kuwa mbunge huyo alihamasisha watu kujipanga na kukataa amri halali iliyokuwa imetolewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, OCD Zuberi Mwombeji, kinyume cha Kanuni ya Adhabu ya 390 na 35.

Mbali na Lema, washitakiwa wengine ni Joseph Simon, Dina Kamtoni, Musa Mwakilema, Jafari Samweli, Juliana Lukumay, Gerald Majengo, Leonard Kiologo, Frank
Daniel, Kelvin Simon na Hassan Mdigo.

Wengine ni pamoja na Lomayan Nasi, Rashid Shumbeti, Amedeus Chami, Daud Hamza, Meshack Betuel, Hamad Shaban, Bahati Daud na Richard Mollel.

Hata hivyo Mbunge huyo amenyimwa dhamana na amepelekwa mahabusu ya Kisongo pamoja nawatuhumiwa wengine.

Watuhumiwa waliokidhi matakwa ya dhamana na kuachiwa na Mahakama hiyo ni Dina, Majengo, Mdigo, Nasi, Shumbeti, Hamza na Daudi.