HATIMAYE kitendawili cha nani ataibuka Malkia wa Dunia 2011, kimeteguliwa kwa Miss Venezuela2011, Ivian Sarcos usiku wa Jumapili Novemba 6, 2011 kufanikiwa kutawazwa kuwa Malkia Mpya wa Taji la Urembo la dunia “Miss World 2011, hulku matumaini ya Tanzania kupitia kwa Miss Tanzania 2011, Salha Izrael Kifai yakigonga mwamba kwa mara nyingine tena katika mashindano hayo.
Katika shindano hilo la aina yake lililofanyika katika ukumbi wa Earls Court in London, Sarcos mwenye umri wa miaka 21 alifanikiwa kuwatupa nje zaidi ya warembo 100 kutoka nchi mbalimbali Duniani katika shindano hilo ambalo lilikuwa ni la 61 tangu kuanzishwa kwake.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa Miss Philippines 2011, Gwendoline Ruais na nafasi ya tatu ikienda kwa Miss Puerto Rico 2011, Amanda Perez.
Bara la Afrika lilifanikiwa kuingiza warembo wawili katika hatua ya makundi ya 15 bora ambapo mrembo kutoka nchini Zimbabwe na jirani zao Afrika Kusini ndio waliolitoa kimasomaso bara hilo.
Afrika tena ikabahatika kuingia katika hatua ya 7 bora ya Miss World pale mrembo kutoka Afrika Kusini alipofanikiwa kuingia katika hatua hiyo.
Shindano hilo lilianza kufanyika saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki lilipambwa na burudani mbalimbali za muziki kutoka kundi la Vijana wa Uingereza la street dance troupe Diversity, wakifuatiwa na utambulisho wa Washiriki wote wa Miss World 2011.
Shindano hilo lilifikia tamati pale Miss World 2010 Alexandria Mills alipopanda jukwaani na kumvika taji Sarcos.
Miongoni mwa majaji wa shindano hilo alikuwa ni washindi wa taji la Miss World ambapo alikuwepo Miss World 1976, Cindy Breakspeare , Miss World 2001, Agbani Darego kutoka Nigeria,Miss World 2007, Zhang Zilin na Miss World 2009, Kaiane Aldorino.

Aidha warembo waliofanikiwa kuingia hatua ya 15 bora ni kutoka nchi za Indonesia, Korea, Italy, Sweden, Zimbabwe, Kazakhstan, Ukraine, Venezuela, Philippines, US VI, Spain, Puerto Rico, Afrika Kusini, Scotland na wenyeji Uingereza.

Huku hatua ya kundi la warembo 7 bora nafasi hizo kuchukuliwa na nchi za Korea, Venezuela, Uingereza , Philippines, Puerto Rico, Afrika Kusini na Scotland.