MUSWADA wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011 umewasilishwa na kusomwa kwa mara ya pili bungeni tofauti na wanaharakati walivyotaka huku madaraka ya Rais yakiendelea kuwepo kama yalivyopendekezwa awali na Serikali.

Mamlaka hayo ni pamoja na Rais kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, kuunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba na kuunda Bunge la Katiba la kutunga Katiba mpya.

Pia atateua wajumbe wa tume hiyo itakayokusanya maoni ambao ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wasiozidi 30. Uteuzi huo utazingatia usawa wa pande mbili za Muungano.

Akisoma madhumuni na muundo wa tume hiyo jana bungeni, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani alibainisha baadhi ya mabadiliko katika muswada huo baada ya Serikali kupokea maoni mbalimbali ya wananchi.

Alisema Rais ni Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na ndiye mwenye mamlaka makubwa hivyo ni vyema Katiba ikasimamiwa na yeye mwenyewe na si mtu mwingine.

Alisema Serikali ilifanya utafiti kuhusu suala hilo na kubaini kuwa si Tanzania pekee inayomtumia Rais katika mchakato mzima wa Katiba kwani nchi kama vile Ghana na Kenya pia katika michakato yao ya Katiba, zilimtumia Rais wao huku Uganda wakimtumia Waziri wa Sheria.

“Ni vizuri tukabadili mtazamo wetu kuhusu Rais, hapa hatazamwi kama Mtawala bali anatazamwa kama Mkuu wa Nchi,” alisema Kombani.

Miongoni mwa mabadiliko katika muswada huo ni pamoja na taasisi binafsi zinazoongozwa na raia wa nje ya nchi hazitaruhusiwa kuhamasisha wananchi kupiga kura za maoni na hiyo ni kuepuka kuingiliwa kwa mchakato wa kuunda katiba mpya.

Watakaoruhusiwa ni vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa nchini na yanayoongozwa na Watanzania na taasisi za kidini. Pia vyama vya siasa vitaruhusiwa kupiga kampeni kwa kushirikiana na tume ya kukusanya maoni.

Muswada huo unabainisha kuwa viongozi wanasiasa wa ngazi zote wakiwemo wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, madiwani, watumishi wa vyombo ya usalama au watuhumiwa ambao shauri lao lipo mahakamani la kukosa uaminifu au maadili, hawatateuliwa katika tume hiyo.

Kwa upande wa Bunge la Katiba, litaundwa na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, mawaziri wenye dhamana ya Katiba ya Serikali ya Muungano na Zanzibar na wanasheria wakuu wa Serikali ya Muungano na Zanzibar.

Pia kuhusu maoni ya kutaka idadi ya wajumbe ipungue, Kombani alisema Serikali imeona hoja hiyo haina nguvu kwa kuwa mchakato wa Katiba unahusisha maeneo mengi na idadi kubwa ya watu hivyo idadi ya wajumbe hao itabaki vilevile 116.

Wajumbe hao ni wale watakaoteuliwa kutoka asasi zisizokuwa za serikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalumu.

Eneo lingine ambalo muswada huo haukubadilishwa kwa mujibu wa maoni ya wadau ni la ripoti ya tume kuhusu mchakato wa Katiba kuendelea kuwasilishwa kwa Rais badala ya kupelekwa bungeni kama ambavyo wadau wengi walitaka.

“Ni dhahiri kuwa ripoti ya tume itawasilishwa kwa Rais kwa kuwa yeye ndiye aliyeunda tume na baada ya hapo ndipo itawasilishwa katika Bunge maalumu,” alisema Kombani.

Kuhusu kubadilika kwa jina la muswada huo, Kombani alisema suala hilo haliwezi pia kubadilishwa kwa kuwa litaondoa dhana nzima na maana ya muswada huo uliolenga kuweka utaratibu wa kukusanya maoni yatakayowezesha kuundwa kwa Katiba mpya.

Kombani alisema wizara yake ilishauriana na Serikali ya Zanzibar na walikubaliana kuwa sheria inayopendekezwa kuunda Tume ya Katiba isiwe ya kudumu na badala yake iundwe tume ya kusimamia kura za maoni.

Aidha alisema pia walikubaliana kuwa Baraza la Katiba lisiundwe na wabunge wote bali liundwe na theluthi mbili ya wabunge wote wa Bunge hilo na wa Zanzibar.

Alisema pamoja na hayo Serikali iliamua kukubaliana na maombi ya wadau ya kutaka kuandaliwa kwa muswada huo kwa lugha ya Kiswahili, ingawa kwa taratibu za Bunge miswada mingi imekuwa ikiandaliwa kwa Kiingereza lakini kujadiliwa na kupitishwa kwa Kiswahili.

Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameshasema Katiba mpya itazinduliwa wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, Aprili 26, 2014.

Sheria hiyo itaruhusu kupigwa kwa kura ya maoni ambapo wananchi watapiga kura ya kutaka au kutotaka Katiba mpya na watakaopiga kura hiyo ni wale waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura. Tume ya Uchaguzi ya Taifa na ya Zanzibar ndizo zitakazosimamia.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Pindi Chana alisema kamati yake inapendekeza katika wajumbe 116 waongezwe wakulima, wavuvi, vyama vya wafanyabiashara na wafanyakazi kwani wao ni wadau pia.

“Kubadilishwe pia badala ya mtu iongezwe taasisi ili mtu au taasisi atakayemkwamisha au kumzuia mjumbe wa tume au sekretarieti kutekeleza kazi yake achukuliwe hatua,” alisema.

Awali kabla ya Waziri Kombani kusoma madhumuni ya muswada huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema wananchi wamepotoshwa na baadhi ya watu kuwashawishi waandamane kuupinga wakidhani muswada huo ndiyo mabadiliko ya katiba.

Alifafanua kuwa muswada huo unatoa nafasi ya kuanzishwa Tume ya kukusanya maoni, Bunge la Katiba na kupigwa kwa kura ya maoni ambapo alisisitiza; “Kutotungwa kwa sheria hii kwa sasa kutachelewesha utungaji wa Katiba mpya.”

Alisema sababu za muswada huo kusomwa kwa mara ya pili ni kutokana na ulishasomwa kwa mara ya kwanza; Kamati ya Katiba ilikusanya maoni ya wananchi katika mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar na maoni mengi ya wananchi yamezingatiwa katika muswada huo.

Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani yaliyowasilishwa na msemaji wa Kambi hiyo, Tundu Lissu, hayakubaliani na mabadiliko yaliyofanywa na muswada huo kulingana na maoni ya wadau na kutaka muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza na si ya pili.

Lissu alisema muswada huo una tofauti kubwa na muswada wa awali hivyo kusomwa kwa mara ya pili ni kosa lakini pia aliendelea kudai kuwa kuendelea kumpa Rais madaraka ni sawa na kuendekeza udikteta.

Baada ya kumaliza kusoma hotuba hiyo, iliyotaka Zanzibar isishiriki kwa usawa katika mchakato huo, wabunge wa Chadema na NCCR walitoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Wakiwa nje, wabunge hao wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, walifanya mkutano na waandishi na kusema wametoka kwa madai kuwa Spika wa Bunge hakuwapa nafasi ya kuzungumza na wakaona kuwa anapendelea upande mmoja.

Aidha Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na Lissu ambao ni wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, walidai waliomba muongozo kutaka hoja hiyo ya katiba ifutwe kwa madai kuwa mjadala mzima wa katiba uliingiliwa na Spika.

Hata hivyo kabla ya kuahirisha shughuli za bunge jana, Spika wa Bunge, Makinda alisema kanuni hazimlazimishi kukubali kila muongozo unaoombwa na mbunge na kuongeza kuwa kwa sasa umekuwa ukitumiwa vibaya na kuonya kuwa atakuwa mkali kukabiliana na hali hiyo.