NDOA ya staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya, ni kizungumkuti, aliyebugia ameshindwa kumeza wala kutema, ni zamu ya mume mtu, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ ambaye ametoa tamko zito.

Uwoya ndiye aliyetangaza kumwagana na mumewe, lakini yamemfika, kwani kauli yake imemrudi, anahaha kuomba msamaha ingawa msimamo na tamko la Kataut, vimemfanya ashindwe kumeza wala kutema alivyobugia.

The 5Star Paper, Risasi Jumamosi, lina utajiri wa taarifa za wanandoa hao, kwani lilizungumza na Kataut pia Uwoya kwa wakati wake.

TAMKO LA KATAUT
Gazeti hili, lilimtia Kataut kwenye 18 zake Alhamisi iliyopita akiwa mtulivu na alipoulizwa kuhusu ‘kibuti’ alichopigwa na mkewe alitoa tamko:

“Mimi sina wasiwasi kabisa, yeye ndiye ameamua. Najua amenidhalilisha kusema hajawahi kunipenda. Amesema ndoa yetu ni kama alilazimishwa, hilo limenisikitisha sana kwa sababu alichosema siyo kweli.

“Tena kwenye suala la kufunga ndoa, yeye ndiye alilazimisha. Alitaka tuwahi kuoana. Nawasikitikia wazazi wake kwa sababu wameingizwa kwenye suala hili ambalo hawahusiki kabisa. Wazazi hawakulazimisha tuoane, ni Uwoya mwenyewe alitaka, tena wakati huo mimi nilikuwa nasita.

“Hata mama yangu amenipigia simu akiniuliza maana alisikia kwenye redio moja nchini Burundi kwamba nimeachana na Irene, anasema habari hii imemshutua moyo.”
WENGINE HUJINYONGA
“Nijinyonge kwa sababu ya mwanamke, hapana, siwezi kufanya hivyo. Nimeshakutana na mambo magumu kuliko hili. Limetokea, najua jinsi ya kukabiliana nalo,” alisema Kataut.

YUPO TAYARI KUMSAMEHE?
“Nimeshasema sina tatizo. Kwanza alikuwa ananipigia simu sipokei kwa sababu ya hasira lakini baadaye nimemwambia aende kwanza kwa wazazi wake akawaombe msamaha. Nimetoa sharti hilo.



“Kuna ‘meseji’ nyingi amenitumia za kuomba msamaha, anataka haya mambo yaishe. Mimi naona huo ni ujinga, alichokifanya Uwoya ni upuuzi mkubwa ndiyo maana nimemwambia badala ya kuja kuniomba msamaha mimi, aende akawaangukie wazazi wake ambao amewadhalilisha,” Kataut.UWOYA HOI
Jumatano iliyopita, baada ya gazeti hili toleo la Jumatano (Risasi Mchanganyiko) kuripoti habari ya ndoa ya Uwoya kuvunjika, ikiwa na kichwa “Ndoa ya Uwoya Yavunjika”, mrembo huyo alipiga simu kwa mwandishi wetu akilia:

“Mama yangu ni mgonjwa sana, niliposema nimeachana na Hamad (Kataut), sikujua kama haya mambo yangefika hapa. Sijui nitafanyaje, sijui alipo na nikipiga simu hapokei.

“Inaniuma sana, mama yangu amepata mshtuko mkubwa (presha) kusikia nimeachana na Hamad. Jamani nampenda sana mume wangu, yale maneno niliyasema kwa hasira na sasa hivi najuta. Yaani ulimi wangu umeni-cost.”

KINACHOMUUMA UWOYA
“Kuna kauli nilisema sijawahi kumpenda Hamad, jamani yale maneno ni hasira. Nampenda sana mume wangu, sitaki kabisa kuachana naye, nitateseka katika maisha haya,” Uwoya.

VIPI KULEA MTOTO BILA BABA?
Uwoya na Kataut wameshapata mtoto mmoja anayeitwa Krish, mrembo huyo anawezaje kuishi na mwanaye bila baba?

“Nitapata shida kumlea mtoto bila baba yake endapo nitaachana moja kwa moja na Hamad. Hata mwanangu nitakuwa simtendei haki, napenda sana apate malezi ya baba na mama kama mimi wazazi wangu walivyonilea.”

UWOYA ALIVYOTAPATAPA

Risasi Jumamosi, linazo SMS za kutosha kutoka kwa Uwoya kwenda kwa Kataut, akiomba msamaha katika dalili kwamba mumewe alikuwa hapokei simu.

SMS ya kwanza ni ile ambayo Uwoya aliituma kwa Kataut wakati akiwa bado na hasira, inasomeka: “Huna lolote, nina habari zako zote, endelea tu na mambo yako.”

Baadaye Uwoya alianza kutapatapa, akamuandikia SMS Kataut: “Baby please nakupenda, please pokea simu.”

Kataut hakupokea, Uwoya akaandika tena: “Baby nimebadilika siku nyingi, please mume wangu, mbona ulishanisamehe? Please baby rudi, naomba tutaelewana tu baby bado nakupenda sana, hakuna mwanaume anayenipenda zaidi yako, nimegundua baby please.”

Pamoja na hivyo, Kataut akaendelea kuwa jiwe, Uwoya akatuma nyingine: “Baby mbona unanifanya hivyo? Nimefanya nini tena? Kama nimekuudhi niambie, mimi mpaka nimempigia baba simu tuonane niongee naye coz kuna demu alinipigia akanitukana sana kisa yeye lakini hakupokea, baby please.”
Uwoya alituma tena nyingine: “Nakusubiri mume wangu mpenzi.”
CHANZO NI HIKI
Gazeti hili limenasa kisa kamili kwamba chanzo cha Uwoya na Kataut kutofautinana ni SMS ya mapenzi.
Uwoya aliliambia Riasasi Jumamosi: “Nilitumiwa SMS nikaambiwa kuna mwanamke tena ni rafiki yangu, anatembea na Hamad, sasa mimi badala ya kutafakari, nikapaniki. Unajua mimi huwa nina hasira za haraka ndiyo maana nikaamua tuachane.”

MAMA UWOYA
Risasi Jumamosi lilifika nyumbani kwa akina Uwoya na kumuona mama yake lakini neno lake ni hili: “Jamani hali yangu siyo nzuri, naumwa, naomba mzungumze na wahusika (Uwoya na Kataut), mimi sina chochote, hali yangu mbaya na sasa hivi nakwenda hospitali.”

UWOYA NA KATAUT WATAWEZA KUELEWANA NA KUMALIZA TOFAUTI ZAO? Usikose kufuatilia hapahapa nitakuletea habari zaidi.


                                                 chanzo