MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati (Cecafa),
Leodegar Tenga (Pichani) amepata mpinzani katika uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo
uliopangwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema Tenga atashindana na Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo, Fadoul Hussein kutoka Djibout.

Wambura alisema Tenga atagombea tena kutetea nafasi yake baada ya kumaliza kipindi cha miaka minne cha kuliongoza baraza hilo ambapo alichaguliwa kwa wadhifa huo mwaka 2007.

Alitaja nafasi nyingine zitakazogombewa katika uchaguzi huo ni za ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya baraza hilo ambapo tayari wanamichezo wanane wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali.

Wambura alisema uchaguzi huo utafanyika siku moja kabla ya kuanza mashindano ya Kombe la Chalenji, ambayo yanatarajia kushirikisha nchi 11.



Wakati huo huo, wachezaji wote wanaocheza soka nchini tayari wamejiunga na kambi ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, inayojiandaa na mchezo wa mchujo wa kuwania nafasi ya
kuingia makundi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Chad utakaochezwa N’djamena Novemba 11.

Akizungumza na waandishi habari jana, Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura aliwataja
wachezaji hao kuwa ni Juma Kaseja, Mwadini Ally, Godfrey Taita, Nadir Haroub, Aggrey Moris, Juma Nyosso, Shaabani Nditi, Hussein Javu, Nurdin Bakari, Ramadhani Chombo,
Mrisho Ngassa, Juma Jabu, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni.

Alisema mchezaji pekee kutoka nje aliyejiunga na kambi hiyo ni Idrissa Rajabu kutoka Sofapaka ya Kenya, wengine walitarajiawa kuingia jana jioni ama leo.