WANAFUNZI sita waliokuwa wakisoma Shahada ya Uzamili, Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni miongoni mwa watu 18 waliokufa Jumamosi katika ajali ya basi la Taqwa lililogongana na lori mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, marehemu hao ni miongoni mwa wanafunzi 10 wa UDSM waliokuwa wakienda Kigali nchini Rwanda kwa ajili ya ziara ya kimasomo katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Kigali.

Kwa mujibu wa taarifa ya Profesa Mukandala kwa vyombo vya habari, wanafunzi waliokuwa katika safari hiyo ni wa kimataifa waliokuwa wakisoma shahada ya uzamili kupitia Programu ya Hisabati katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki.

Miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo, wawili ni raia wa Malawi, Watanzania wawili, Mganda na Mzambia.

Watanzania waliokufa ni Nshaija Muganyizi, na Kassim Dadi, Wamalawi ni Chikondi Chasowa na Josephine Kaleso, Mganda ni Mubiru Patrick na Mzambia ni Chimuka Hamajata.

Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa UDSM, Jackson Isidory, marehemu mmoja atazikwa kwao Bukoba, mwingine atapelekwa Uganda kama Idara ya Uhamiaji itaruhusu wengine wataletwa Dar es Salaam leo.

Kwa mujibu wa Isdory, wanafunzi watatu walioumia waletwa Dar es Salaam ili watibiwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Rose Mara, John Andonisye na Mwale Moses.



Basi la Taqwa lenye namba za usajili T 635 ABC aina ya Nissan Diesel lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Bujumbura Burundi liligongana na lori la Kampuni ya Bakhresa lenye namba za usajili RAB 255ACT lililokuwa likitoka Ngara kwenda Dar es Salaam.

Magari hayo yaligongana Jumamosi saa nne asubuhi katika eneo la Lusahunga wilayani Biharamulo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Salewi aliwataja miongoni mwa waliokufa kuwa ni Chimuka Hamajata, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye ni raia wa Zambia anayeishi Kitwe.

Wengine waliokufa ni dereva wa basi hilo, Sultan Mohamed (36), mwenyeji wa Kahama mkoani Shinyanga, Ruzindana Theonest (35) aliyekuwa dereva wa lori na raia wa Rwanda.

Marehemu wengine ni Erick Eliud (18) mwenyeji wa Wilaya ya Ngara, Ally Issa (35) mkazi wa jijini Dar es Salaam, Aziza Said (60), Habiba Juma (45) na Farida Abdalah (35) wote wakazi wa Mkoa wa Tabora.

Kamanda Salewi alisema katika ajali hiyo iliyotokea katika barabara ya Lusahunga – Nyakahura, abiria 11 walikufa katika eneo la ajali na kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wa magari yote mawili.

Aliwataja majeruhi waliokuwa wamelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo ni Joseph Baltazari (24) mkazi wa Ngara, Said Suleiman (4) mkazi wa Tabora na Ntabenda Anicet (29) raia wa Burundi.

Wengine ni Andongwisye Mwakisisile (39) Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Donald Richard (20) mkazi wa Ngara, Joseph Bigilimanyu (34) raia wa Burundi, Pina Elisha (12) mkazi wa Ngara na Jane Kasanga (46) mkazi wa Tabora.

Aliwataja waliolazwa katika Hospitali ya Omulugwanza wilayani Ngara ni Ajintha Sewitha (53) na Samwel Rusulo (46) wote wakazi wa Ngara. Wengine ni Albert Dafura fundi seremala mkazi wa jijini Dar es Salaam na Kabula Ismail (27) mkazi wa Bujumbura nchini Burundi.