Watu wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Singida kwa tuhuma za kumiliki noti bandia zenye thamani ya sh 1,730,000.
Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Singida, SSP Ayoub Tenge, alisema noti hizo bandia zote zilikuwa za shilingi elfu tano na elfu kumi na kuwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa ni pamoja na Lucas Mpinga (50), mkulima na mkazi wa kijiji cha Ndala, tarafa ya Kinyagiri na Daudi Enock (30), mkulima wa Kijiji cha Kisana, kata ya New Kiomboi.
Alisema katika tukio la kwanza lilitokea Novemba 8 saa 9, alasiri katika mnada wa Iguguno, kata ya Iguguno, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa anamiliki noti kumi bandia za elfu tano zenye thamani ya sh 50,000.
Hata hivyo, Tenge alifafanua kwamba mtuhumiwa Daudi ambaye pia ni mfanyabiashara wa samaki alikutwa na noti tatu za elfu tano zenye namba inayofanana za Bx 4086370 na noti zingine mbili zenye namba BD D100090 na AC 0004714. 
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi katika tukio la pili, Lucas alikutwa akimiliki noti bandia zenye thamani ya sh 1,680,000.
“Inasadikika kuwa mtuhumiwa huyo aliuza gunia za mahindi 42 kwa mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Yasini Amri akiwa na wenzake ambao hata hivyo walitoroka na kutelekeza mahindi hayo baada ya kubaini kuwa walikuwa wanafuatiliwa na polisi na bado jitihada za kuwasaka watuhumiwa hao zinaendelea,” alisisitiza.

Kaimu kamanda huyo hata hivyo alizitaja noti bandia za elfu kumi kwamba zilikuwa na namba BU 2232220, 7232222, 7332224, 7232225, 7232226, 7232227, 7232229, BL 3263376, 3263378, 3263379,BT 5532739 na 5532734 za elfu tano tano ni BH 0012030, 0012031, 0012032, 0012033 na 0012036 na kwamba baadhi namba za noti hizo bandia zinafanana. Tenge alisema pia kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa ili kupata chanzo cha noti hizo bandia zinakotegenezwa.
Kaimu kamanda huyo hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha wananchi kuwa makini na malipo ya noti bandia na kwamba wajenge utamaduni wa kuchunguza fedha wanazopewa ili kuondoa uwezekano wa kupata hasara.