WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amekitaka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiache uanaharakati na maandamano ya mara kwa mara kama kinataka nchi isonge mbele.

Pinda alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge katika mkutano wa tano wa bunge unaoendelea, Dodoma, akisema Chadema inahitaji kuteremka chini na kuangalia maslahi ya nchi kwa mapana zaidi.

Alielezea kukerwa na mtindo inaoutumia wa kufanya maandamano kila kukicha na kaulimbiu yao ya ‘Peoples power (Nguvu ya umma)’ kwamba hazioneshi dhamira ya kweli ya kuleta amani.

Alisema ipo haja kwa Chadema kubadilika, ili kuipa imani Serikali kukiona kuwa ni chama makini na kinachohitaji kumaliza mgogoro uliopo.

Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) aliyesema kuwa mgogoro wa vyama vya CCM na Chadema wa umeya wa Arusha umevuka mipaka na kusambaa nchi nzima na kuwa wa kitaifa.

“Hivi sasa (mgogoro huo) umevuka mipaka ya kivyama na umekuwa wa kitaifa na kusambaa maeneo mbalimbali ya nchi na kwa kuwa (Pinda) ulilitambua hilo na ukaandika barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na baada ya kupokea majibu ya CCM je, upo tayari kutoa maelekezo mengine ama ushauri mwingine ili upande wa pili ujue hatima ya suala hili na ijue hatua za kuchukua?” Alihoji Mnyika.

Pinda alijibu; “Ndugu Mnyika usilikuze jambo hili kama limesambaa nchi nzima, si kweli, lakini kikubwa ninachokiona katika mazingira ninayoyaona, wenzangu wa Chadema mnayoyafanya kinachohitajika ni dhamira ya kweli kwa pande zote mbili, kwa namna mambo yenu mnavyoyafanya huoni dhamira ya kweli.



“Kila siku maandamano kila mahali sisi tulioko serikalini tunapata tabu sana, tunataka kufanya kazi nyingine ambazo zinahitajika, lakini muda wote unakaa unafikiria maandamano.

“Mteremke chini kidogo, tuanze kuona maslahi mapana ya nchi, tuone ni mambo gani ya msingi yanahitajika, kwa pamoja twende mbele,” alisema.

Alisema tabia ya uanaharakati ya Chadema inanipa taabu sana, lakini kama umakini utakuwapo, haoni tatizo watu kukaa na kuzungumza suala hilo, “katika hali ninayoiona mimi ‘peoples power’ kila kukicha si nzuri, haiwezekani.”

Kuhusu mgogoro wa umeya wa Arusha, Pinda alisema kama Chadema inaona haja ya kukaa kwa mazungumzo iandike na kuelezea maeneo inayoyaona yanahitaji kujadiliwa.

Awali Pinda alieleza kuwa aliingilia mgogoro huo kwa kumwelekeza Msajili akutane na vyama hivyo, kuona maeneo ya kuzungumza akiamini tatizo litapatiwa ufumbuzi lakini CCM ilijibu kwa barua kwamba haioni cha kuzungumza.

Akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), aliyetaka kufahamu kwa nini Serikali imemzuia Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kutoka rumande na kuathiri utalii, alisema Mbunge huyo hakuzuiwa bali mwenyewe alikataa dhamana.

Alisema wanatarajia Novemba 14 kesi hiyo itakapotajwa, Mbunge huyo anaweza kuachiwa na kuongeza kuwa utalii haujaathirika kutokana na vurugu hizo, lakini akawataka wananchi kuzingatia amani ili utalii huo usiathirike.