MWANAMUZIKI wa kizazi kipya na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu anatarajiwa kuwapawisha mashabiki wa muziki huo jijini Arusha.  
Sugu akiwa na wasanii wengine wanatarajiwa kukonga nyoyo za mashabiki katika viwanja vya Tripple A mjini hapa kwa kiingilio cha Sh. 5,000.
 
Akizungumza na vyombo vya habari jana mjini hapa Sugu aliwaomba wakazi wa Jiji la Arusha kujitokeza na kuwaunga mkono wanamuziki walioamua kufanya harakati za kupambana na kuukomboa muziki wa kizazi kipya.

“Tamasha hili la “Anti Virus Burudani kwa mashabiki” linalenga kupiga kelele au kufikisha ujumbe kwa Taifa ili watoke nje na kuungana na wasanii katika kutetea kazi zao.

“Kwa miaka mingi wasanii wamekuwa wakilalamika kwenye nyimbo. Lakini sasa tumerudi jukwaani kuonyesha bado wasanii hawajaishiwa kama inavyodaiwa,” alisema Sugu.

Akielezea matamasha mengine yatakayofuatia alisema baada ya kuzindua Dar es Salaam Novemba 18 Mwaka huu, Anti Virus itapelekwa Jiji la Mbeya Desemba 24 Mwaka huu na baada ya hapo itakwenda Morogoro kisha Jiji la Mwanza.

“ Nia yetu ni kuipeleka Anti Virusi nchi znima ili kuwatia moyo wasanii wa maeneo ya mikoani mbali na Dar es Salaamu,” alisema Mr. Sugu.

Hata hivyo Sugu alibainisha kuwa jambo moja analojivunia ni kuona wasanii wakubwa na wenye majina katika muziki nchini wakimuunga mkono kwa kuamua kujitoa muhanga kuibeba sanaa hiyo.
“Asilimia 99. 9 ya wasanii wenye majina makubwa nchini wanatuunga mkono, hatuwezi kuweka wazi mawasiliano hiyo ni siri unajua haya ni mapambano.

Baadhi ya wasanii waliotajwa kuonyesha vimbwenga vya siku hiyo ni pamoja na Suna G, Adili, Mkoloni, Mapacha, Dany Msimamo,Peen Lawyer, D wa Gheto, Coin, Soggy Dogy, Rama Dee, Mr. Sugu mwenyewe na Isanga Family.
(na father kidevu)