Na Kadija Mngwai
KOCHA Msaidizi wa Kilimanjaro Stars, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema kipa wa timu hiyo, Juma Kaseja (pichani), amechoka kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo, hivyo, anatakiwa apumzike.

Akizungumza na Championi Jumatano, Julio alisema uwezo wa Kaseja umepungua kwa kiasi fulani kutokana na kushindwa kupata muda mrefu wa kupumzika.

“Amecheza mechi nyingi mfululizo bila ya kupumzika katika michuano mbalimbali ikiwa ni pamoja na mechi za Ligi Kuu ya Bara, hivyo, anatakiwa apumzike ili aweze kuimarisha kiwango chake, lakini tatizo ni kwamba, hakuna kipa mwenye kiwango kama chake.

“Hii ndiyo sababu kubwa ya kuweza kumtumia mara kwa mara kila anapokuwa katika kikosi cha timu ya taifa. Iwapo angekuwa anapata muda mwingi wa kupumzika, angekuwa kipa tishio zaidi,” alisema Julio.

Kaseja amekuwa chaguo la kwanza la Simba katika misimu zaidi ya mitatu mfululizo na amekuwa akikaa langoni kwa mechi zote ambazo anakuwa hana majeraha, hali hii imetokea pia katika mechi za timu ya taifa kila anapoitwa.