WATU waliokuwa wakizika katika makaburi ya Nyihogo wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, wameokota risasi 691 za bunduki aina ya SMG zilizokuwa ndani ya kaburi la mtoto mchanga lililokuwa halijafukiwa.

Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, tukio hilo lilitokea juzi saa kumi jioni wakati wananchi hao walipokwenda kuzika mwili wa babu mmoja aliyefariki katika Kijiji cha Mhungula.

Walidai baada ya kuuchukua mwili wa marehemu huyo na kwenda kumzika katika makaburi hayo, ghafla waliona kaburi lililokuwa pembeni la mtoto mchanga likiwa wazi huku mwili wa marehemu ukiwa na sanda na pembeni kukiwa na mfuko ambao ndio uliokuwa na risasi hizo 691.

Mmoja wa mashuhuda hao, Maganga Kapela alisema baada ya kuona mfuko huo, ndipo waliufungua na kukuta risasi hizo na kupiga simu kwa Polisi, waliofika na kushiriki katika maziko hayo, kisha kuzichukua risasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani amethibitisha kuokotwa kwa risasi hizo na kuahidi kuwa maelezo zaidi atayatoa pindi watakapomaliza uchunguzi juu ya tukio hilo