Nyota wa muziki wa kizazi kipya Roma Mkatoliki na Fid Q walikuwa kivutio kikubwa wakati walipotoa shoo kali katika tamasha maalum la kusherehekea miaka 50 ya Uhuru lililofanyika katika Ufukwe wa Coco Beach jijini Dar es Salaam.
Wasanii hao walizikonga nyoyo za umati mkubwa wa watu uliohudhuria katika tamasha hilo kwa umati huo kuimba wakiwafuatisha wanamuziki hao ambao walipanda jukwaani kutoa burudani kwa nyakati tofauti.
Mbali na wasanii hao, wanamuziki wengine waliotoa burudani katika tamasha hilo ni kundi la Tip Top Connection, Twenty Percent, Godzilla na wasanii wengine wanaochipukia katika muziki wa kizazi kipya.
Tamasha hilo lililofanyika kwa siku mbili mfululizo (Jumamosi na Jumapili) liliandaliwa na kampuni ya huduma za simu ya Tigo ikiwa na lengo la kusherehekea miaka 50 ya Uhuru kama sehemu ya kutoa shukrani kwa wateja wake.
Akiongea wakati wa tamasha hilo, mwakilishi wa Tigo, Benny Lutaba alisema kuwa tamasha hilo liliwapa nafasi pia wateja wa Tigo kupata bidhaa mbalimbali pamoja na huduma nyingine za Tigo kwa bei nafuu. “Siku hizi mbili wateja wetu wamepata burudani ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru na pia kupata fursa ya kujipatia huduma zetu kwa bei nafuu,” alisema.