Imani Makongoro
BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Francis 'SMG' Cheka ametamba 'kumfunga mdomo' mpinzani wake Karama Nyilawila katika pambano lao lisolokuwa la ubingwa la uzani wa Kati litakalofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Cheka ambaye atapanda ulingoni Januari 24 kuzipiga na Nyilawila katika pambano la raundi 10 alisema alikuwa akimhofia Nyilawila, lakini kutokana na mazoezi aliyofanya anaamini lazima Nyilawila atasalimu amri.

"Nyilawila ni bondia mzuri na ana rekodi ya kufanya vizuri katika mapambano mbalimbali, lakini pia ni bondia ambaye naweza kusema nilkuwa namvutia muda tu na wakati wake wa 'kunipigia saluti' umewadia," alisema Cheka.

Alisema uwezekano wa bondia huyo kumaliza raundi zote 10 upo endapo tu atafanya mazoezi mara tatu zaidi ya anayofanya siku zote ama sivyo mpinzani wake huyo atarajie kipigo cha Knock Out (KO).

"Najikubali mimi ni bondia ambaye naweza pia, ni wa kwanza kuwa na mashabiki wengi hapa nchini hivyo ili nisishushe heshima yangu ni lazima Nyilawila afuate nyayo za mabondia wenye rekodi ya kupigwa na Cheka," alisema.
Bondia huyo ana rekodi ya kufanya vizuri hapa nchini huku akiwa na historia ya kumkung'uta Mada Maugo kwa pointi zaidi ya mara moja na kumtandika Japhet Kaseba katika pambano lililofanyika jijini Dar es Salaam.