Kenya inasema kuwa itawashambulia wapiganaji wa Kiislamu ndani kabisa kusini mwa Somalia.
Msemaji wa jeshi la Kenya, Kanali Cyrus Oguna, alisema mashambulio ya ndege zao yatalenga bandari za nchi hiyo, pamoja na mji wa Afgoye, karibu na Mogadishu, na ambako maelfu ya watu waliohama makwao wamekimbilia.
Aliwaonya watu wajaribu kuwa mbali na maeneo ya al-Shabaab. 
Wanajeshi wa Kenya wako katika maeneo matatu ya kusini mwa Somalia, lakini hawakusonga mbele tangu kuingia huko mwezi wa Oktoba.
Kanali Oguna alisema Kenya haitasita hadi imefanikiwa kufikia malengo yake:
"Tunachosema ni kuwa tutaweza kuwaandama Al-Shabaab popote pale wanapokwenda.
Na ni haki kuyalenga maeneo ya Al-Shabaab, ikiwa wapiganaji hao wanasonga au wako pahala pamoja.

Popote pale waliko Al-Shabaab, tukishawatimua, tutaliteka eneo lao, hadi Kenya itapohisi iko salama.
Hivi sasa tunahusika zaidi na kuleta usalama.
Na nataka kusisitiza kuwa kurejesha usalama ni sehemu muhimu ya shughuli zetu, na pamoja na kutoa msaada wa kiutu.
Kurejesha usalama ni kazi ngumu, inataka jitihada na inachukua muda.
Lakini tukiwa na hakika kuwa tumerejesha usalama wa kutosha katika maeneo tuliyoteka, tutasonga mbele."BBC