Leo ni miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Hata hivyo, shamra shamra za kufikia kilele zilianza muda na jana kulikuwa na mkesha nchi nzima ulioandamana na mapambo ya kila namna. Hapa ni eneo maarufu la Mnara wa Askari jijini Dar es Salaam likimeremeta jana usiku na kubadilisha mandhari yake yaliyozoeleka ikiwa ni sehemu ya kukaribisha siku hii muhimu ya leo. (Picha na Robert Okanda).

TANZANIA Bara leo inatimiza miaka 50 ya Uhuru, huku ikijivunia mafanikio mbalimbali katika nyanja za elimu, afya, miundombinu na zaidi ujenzi wa taifa uliodumisha umoja na udugu wao.

Katika maadhimisho hayo ya kipekee, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kukagua gwaride la heshima litakaloongozwa na vikosi vya
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Akizungumzia maandalizi ya shughuli hiyo juzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said
Sadiki alisema mbali na gwaride, pia kutakuwa na burudani za aina mbalimbali vikiwemo vikundi vya sanaa, tarumbeta na sherehe hizo zitapambwa na vijana wa halaiki.

“Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa nchi yetu ni tukio kubwa na la kihistoria, hivyo natoa
mwito kwa wakazi wote wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru ili
kushuhudia tukio hilo kubwa na la kihistoria ambalo huenda wengi wetu hatutapata bahati ya
kuliona tena,” alisema.

Kwa takribani wiki moja sasa wizara, taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali na kampuni binafsi zilishaanza kufanya maonesho ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru tangu Desemba mosi
katika viwanja vya Mwalimu Nyerere ili kuwaonesha wananchi shughuli mbalimbali wanazozifanya.

Kabla ya maonesho hayo, wizara hizo pia zilifanya maonesho mengine katika viwanja vya
Mnazi Mmoja kwa takribani wiki moja kila wizara.

Kama kawaida milango ya Uwanja wa Uhuru leo itafunguliwa asubuhi na mapema ili kuruhusu
wananchi kuingia na kujipanga kabla ya kuwasili kwa wageni waalikwa na viongozi mbalimbali.

Baada ya kuwasili kwa viongozi wote, Rais Kikwete anatarajiwa kuingia uwanjani hapo na
kupigiwa Wimbo wa Taifa na mizinga.

Baada ya hapo Rais Kikwete anatarajiwa kukagua gwaride la heshima ambapo baadaye
gwaride hilo litapita mbele yake kwa mwendo wa pole na wa kasi.

Moja ya vivutio vikubwa katika maadhimisho ya mwaka huu ni pamoja na kupita kwa baadhi ya magari na vifaa vya kivita vikisindikizwa na ndege za abiria na ndege vita.



Akizungumza jana na gazeti hili, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na
Bunge, William Lukuvi alisema baadaye katika sherehe maalumu itakayofanyika Ikulu, Rais Kikwete atatoa kamisheni za heshima kwa baadhi ya maofisa na askari wa vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama.

Akielezea baadhi ya mafanikio ya Uhuru jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen-Kijo Bisimba alisema mbali na changamoto ya umasikini, lakini kumekuwepo mafanikio katika nyanja ya haki za binadamu.

“Huu ni mwaka wa 50 tangu nchi yetu ipete Uhuru, yapo mambo mazuri yaliyopatikana katika
nyanja hiyo kama vile kuwepo na hati za haki za binadamu katika Katiba na pia Serikali yetu kuridhia mikataba karibu yote muhimu ya haki za binadamu,” alisema Hellen.

Mmoja wa wanasiasa wa siku nyingi, Dk. Chrisant Mzindakaya alisema nchi imepata mafanikio
mengi ikiwemo kwenye afya, elimu, kilimo, miundombinu na sekta nyingine, lakini ingeweza
kupiga hatua zaidi kama sera ya mwanzo ya Uhuru ni Kazi ingetumika.

‘’Kuna mabadiliko mengi sana ukilinganisha na mwanzo, watu wengi wamejikita kwenye biashara ingawa hawajajikita kwenye masuala ya uzalishaji.

“Misingi ya nchi ni maendeleo na hakuna maendeleo pasipo kufanya kazi kwa bidii. Umoja na
muongozo mzuri katika mashirika binafsi na ya Serikali lazima usimamiwe vizuri ili kuifanya nchi isonge mbele kwani ndio chanzo cha maendeleo,’’ alisema Mzindakaya.

Salamu za pongezi, wageni mbalimbali
Akitoa salamu zake kwa Rais Kikwete, Malkia Elizabeth wa Uingereza, alisema Tanzania
inasherehekea miaka 50 ya kujitawala kwa amani na utulivu.

“Inanipa faraja kubwa kukutumia wewe Mheshimiwa Rais na watu wa Tanzania pongezi katika
siku hii muhimu,” alisema Malkia.

Alisema Mtoto wa Mfalme wa Uingereza na mkewe waliotembelea Tanzania hivi karibuni kama sehemu ya sherehe hizo, alimueleza namna alivyofurahia ukarimu wa Watanzania.

“Nakutakia wewe Mheshimiwa Rais na Watanzania mafanikio mema katika miaka ijayo,” alisema Malkia.

Mbali na Malkia Elizabeth, pia Rais Barack Obama alishatoa salamu zake za pongezi kwa Rais Kikwete na Watanzania. Wakati huo huo, taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zilieleza kuwa viongozi mbalimbali walikuwa wakiwasili.

Mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni jana miongozi mwa wageni waalikwa waliokuwa
wameshawasili ni Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba, Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika, Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza.

Wengine ni Rais wa Bunge la Korea, Kim Jong Nam, Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel
Aziz na Rais wa Comoro, Ikililou Dhoinine pamoja na Rais mstaafu wa nchi hiyo, Ahmed Abdallah Mohamed Sambi.