MAJAMBAZI watatu wakitumia usafiri wa pikipiki maarufu jijini Arusha kwa jina la ‘toyo’ au maarufu nchini kama bodaboda, wamempora dereva wa gari la hoteli maarufu ya kitalii ya hapa, Kibo Palace na kuondoka na Dola za Marekani 200,000 (zaidi ya Sh milioni 320).

Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi na kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Akili Mpwapwa, zilieleza kuwa uporaji huo ulifanywa Desemba 15, mwaka huu kati ya saa 4 na 5 asubuhi.

Mpwapwa alisema tukio hilo la ujambazi halijafika rasmi mezani kwake, lakini lipo mikononi mwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha (RCO) kwa uchunguzi zaidi na likikamilika atalitolea taarifa.

“Kwangu hilo suala halijafika na siwezi kukupa kitu kwani sina takwimu zozote, lakini liko kwa RCO, akikamilisha atalileta kwangu na nitakuwa katika nafasi nzuri ya kulielezea kwa undani zaidi,” alisema.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia uporaji huo wa fedha za kigeni, walidai majambazi hao walilizuia gari hilo mita chache kutoka katika hoteli hiyo iliyopo katika Barabara ya Old Moshi kwa toyo na kujifanya wamegongwa na gari hilo.



Habari zilieleza kuwa baada ya majambazi hao kuizuia gari hiyo kwa staili hiyo na kudai kugongwa na gari hilo, dereva aliteremka kuangalia kama kweli amewagonga, ndipo mmoja alikwenda moja kwa moja kufungua mlango na kuchukua kifurushi hicho cha fedha za kigeni.

Mashuhuda hao ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao, walidai baada ya kufanya uporaji huo, majambazi wawili walivamia moja ya gari na mwingine alitokomea na toyo, lakini gari lilikutwa eneo la Sinoni nje kidogo ya Jiji la Arusha likiwa limetelekezwa.

Habari zilisema kuwa gari hilo aina ya Vx lililokuwa halina namba za usajili, lilitelekezwa Sinoni nje ya nyumba ya mtu aliyetambuliwa kwa jina la Richard Malesi na majambazi hao kutokomea kusikojulikana.

Mmiliki wa nyumba hiyo, Richard Malesi alipiga simu polisi kueleza gari hilo lililotelekezwa nje ya nyumba yake na polisi walipokwenda kulichukua, alikamatwa mmiliki wa nyumba na kulazwa ndani kwa siku tatu na juzi kutolewa kwa dhamana na uongozi wa Kituo Kikuu cha Polisi.

Hata hivyo, habari zilieleza kuwa dereva wa gari hilo ambaye jina lake halijapatikana na watumishi wengine wawili wa hoteli hiyo wanashikiliwa na Polisi.

Habari za kipolisi zinaeleza kuwa uporaji huo unatia shaka kwani hakukuwa na silaha yoyote iliyotumika na upelekaji wa fedha hizo benki ulikuwa wa kienyeji sana kuliko kawaida kinyume cha maagizo ya Jeshi la Polisi kutaka wenye fedha nyingi ambao wanataka kupeleka fedha benki lazima wapate ulinzi wa polisi.