MKAZI wa Mazwi mjini Sumbawanga, Yusuph Ahmad 'John' (20) ambaye anatuhumiwa kumuua mwalimu wa Shule ya Msingi Kianda, juzi alizua kizaazaa baada ya kufanikiwa kwa
muda kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa mchana mjini hapa . Mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake
anadaiwa kumuua kwa kumnyonga mwalimu Richard Emilly (50) katika kitongoji cha
Chiluba kilichopo eneo la Mazwi mjini hapa.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Isuto Mantage amethibitisha kukamatwa tena kwa mtuhumiwa huyo na anatarajiwa kupandishwa kizimbani kesho baada ya upelelezi wa awali kukamilika.

Inadaiwa kwa ushirikiano wa raia wema mtuhumiwa huyo aliweza kukamatwa na askari Polisi
huku wenzake wakidaiwa kufanikiwa kutoroka na kujificha kusikojulikana, lakini muda mfupi
baada ya kufikishwa kituo cha Polisi mjini hapa kwa mahojiano akiwa chini ya ulinzi mkali wa
polisi aliweza kutoroka na kuanza kukimbia.

Hali hiyo ilisababisha kizaazaa mjini hapa hususani maeneo hayo ya kituo cha Polisi pale wananchi walipojitokeza na kushuhudia mtuhumiwa huyo akichanja mbuga akielekea eneo la Hospitali ya Mkoa huku polisi wakipuliza filimbi wakiashiria kutoroka kwa mtuhumiwa huyo.

“Sijawahi kuona `live’ nimezoea kuona kwenye video leo nimeshuhudia; ilikuwa kama kuona mkanda wa video mtuhumiwa huyo baada ya kutoroka alianza kukimbilia eneo la Hospitali
ya Mkoa huku wengi wetu tukiwa tumepigwa na butwaa kwa muda,“ alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina moja la Jackson, mkazi wa eneo la Kizwite mjini hapa.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa baada ya kufika eneo hilo la Hospitali ya Mkoa aliparamia ukuta
uliozunguka eneo la hospitali hiyo ambapo alishukia ndani ya eneo la hospitali na kisha akapanda juu ya mti mrefu uliopo kwenye eneo hilo na kujificha kwenye matawi yake.

Huku akiwa amejificha kwenye matawi mtini, polisi wenye silaha waliosheheni kwenye magari kadhaa kukabiliana naye walifika eneo hilo la hospitali na kuanza msako mara moja bila mafanikio.



Wakiwa wamekata tamaa na kujiandaa kuondoka eneo hilo ndipo mtuhumiwa alipojirusha kutoka mtini na kutua kwenye paa la moja ya majengo hospitalini hapo.

Mwandishi wa habari hizi naye alifika eneo hilo na kushuhudia mtuhumiwa akiwa anajirusha kutoka mtini na kutua salama kwenye paa la jengo mojawapo hospitalini hapo ndipo umati uliokusanyika eneo hilo walipoanza kupiga kelele wakionesha alipo mtuhumiwa.

“Wote tulijua ameondoka eneo hili la hospitali nadhani aliingiwa na hofu akidhani tumemwona
kumbe wapi, kama angevumilia kujificha kwenye matawi yale ya mti ule hadi usiku halafu akaamua kushuka hakuna ambaye angeweza kumshuku,“ alisikika akisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Mtuhumiwa aliwekwa tena chini ya ulinzi mkali huku akipata mkong’oto wa nguvu kutoka kwa
askari Polisi.

“ Bila shaka wamemuumiza sana vipi kama wangemchukua tu bila ya kumpiga kikatili vile? “

Alihoji mmoja wa mashuhuda aliyekerwa na kitendo cha askari Polisi kuanza kumpatia kipigo mtuhumiwa huyo.

Kamanda Mantage alisisitiza kuwa, Polisi inaendesha msako mkali ili kuwabaini watuhumiwa
wengine wanaohusika katika mauaji ya mwalimu huyo.