Dustan Shekidele, Morogoro na Mtandao

Hatimaye mwakilishi wa Bongo katika shindano la Big Brother Africa ‘All Stars’ 2010, Mwisho Mwampamba (pichani), amefunga ndoa na mshiriki mwenzake, Meryl Shikwambane wa Namibia, Risasi Jumamosi limeinasa.

Kwa mujibu wa habari zilizopamba mitandao na vyombo vya habari nchini Namibia mwanzoni mwa wiki hii, Desemba 10, mwaka huu, Mwisho na Meryl waliungana na kuwa mume na mke huko Parliament Gardens Windhoek nchini Namibia.

TAYARI WANA MTOTO
Habari hizo ziliweka ‘pleini’ kuwa tukio hilo lilihudhuriwa na watu maarufu nchini humo, kufuatia ustaa wa Meryl ambaye miezi kadhaa iliyopita alijifungua mtoto wa Mwisho na kumpa jina la Monkey.

MZEE MWAMPAMBA AFUNGUKA
Baada ya kuzitia kibindoni habari hizo, ‘polisi’ wetu alisaga soli hadi ofisini kwa baba mzazi wa Mwisho, Dk. Ephraim Mwampamba katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Morogoro ambapo alikiri mwanaye kumuoa Meryl.

“Ni kweli Mwisho amemuoa Meryl Jumamosi iliyopita huko Namibia, lakini sikwenda, nilimtuma kaka yake. Hata hivyo, alinionyesha heshima kubwa kwani alimleta Meryl nyumbani, wakakaa wiki mbili kisha wakaondoka.” 
  
TUJIKUMBUSHE
Muunganiko wa wawili hao unatokana na ahadi aliyoiweka Mwisho kwa Meryl wakiwa katika mjengo wa Big Brother, ambapo alimvalisha pete ya uchumba.
Hiyo inadhihirisha ni jinsi gani shindano hilo linawakutanisha watu wa mataifa mbalimbali na kuwaunganisha.

Unakumbuka uhusiano wa Abergail Brigette Plaatjies ‘Abby’ na Gaetano Juko Kagwa wa mwaka 2003? Wote ni wa mataifa tofauti.
Aidha, Big Brother Africa 2007, Richard Bezuidenhout wa Tanzania na Tatiana Durao wa Angola waliwahi kuripotiwa kutoka kimapenzi.
Ndoa ya Elizabeth Gupta aliyeiwakilisha Tanzania mjengoni mwaka 2009 na aliyeshinda taji hilo, Kevin Chuwang wa Nigeria, ni uthibitisho kuwa Big Brother Africa ni kiungo cha uhusiano wa kimapenzi kwa washiriki.
                                                                      GPL