Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya akielekea ukumbi wa mikutano wizarani kuzungumza na baadhi ya watendaji wakuu wa wizara na waandishi wa habari. Kushoto ni mwanawe, Emmanuel Mwadosya. (Picha kwa hisani ya Wizara ya Maji).

“BAADA ya kutangazwa tanzia kwamba Profesa Mark Mwandosya, amefariki dunia, leo nipo
hapa mbele yenu. Si mzimu, si kwamba nilikufa halafu sasa nimefufuka kama ilivyokuwa kwa Lazaro, hapana mimi sikufa nilikwenda India nikiwa hai na nimerejea hai.

“Kwa miaka 34 ya utumishi wangu serikalini, sikuwahi kuumwa kiasi cha kunifanya nilazwe
hospitali, lakini safari hii nimeugua na kupelekwa India kwa matibabu.“Nimekaa India kwa miezi mitano na nusu, kitanda cha kwanza kulazwa imekuwa ni India.

Kilikuwa ni kipindi kigumu na cha mateso kwangu lakini namshukuru sana Mungu kwa yote.
Hayo ni maneno ya utangulizi ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya alipokutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza jana na waandishi wa habari na watendaji wa juu wa Wizara yake tangu arejee kwenye matibabu katika Hospitali ya Apollo, India, Jumanne.

Akiwa amesubiriwa kwa zaidi ya saa moja kwenye chumba cha mkutano cha Wizara yake, saa tano na dakika kumi asubuhi, Profesa Mwandosya alionekana akishuka kwenye gari akitembea kwa kusaidiwa na mkongojo (fimbo maalumu), hali yake ikionekana imeimarika.

“Naonekana natembea kwa kushika gongo au fimbo, si tatizo kubwa naweza kusema huu ni mwendo wa madaha na maringo, hali hii itadumu kwa muda mfupi na baadaye nitajiunga tena na timu yetu ya soka ya Wizara ya Maji tayari kushindana na wizara nyingine…naamini
nitacheza vizuri na nitawezesha kushinda.”

Matibabu akiwa India
Waziri Mwandosya ambaye alizushiwa kifo akiwa India alitumia nafasi hiyo ya pekee kuelezea namna alivyougua hadi kupona ugonjwa ambao alikataa kuutaja na kudai ni siri baina yake na daktari wake.

“Ukiwa mgonjwa utajua uliishi vipi na watu. Ugonjwa wangu ulikuwa na faraja kubwa sana
kutokana na salamu, sala na dua nilizokuwa naombewa. Dua na maombi ni sehemu muhimu
sana kwa mgonjwa maana zinasaidia katika uponyaji wa kiroho zaidi kuliko kimwili.

“Nilikuwa napokea simu nyingi sana, meseji, kadi za salamu kwa njia mbalimbali. Upendo
na ubinadamu niliooneshwa ni wa kiwango cha juu sana na ambao sikuutegemea. Nilipata salamu kutoka kwa wananchi wa kawaida kabisa ambao waliniombea bila kujali tofauti za dini
wala itikadi za siasa. Mungu amesikia maombi yao nimerejea nikiwa salama.”



Waziri Mwandosya alisema pamoja na salamu hizo nyingi zipo zilizotoka kwa viongozi wa
juu wa Serikali, viongozi wa dini na siasa, alimtaja Rais Jakaya Kikwete kama mfariji wake wa
kwanza kutokana na kumpigia simu mara kwa mara na kumtia moyo.

“Si nia yangu kuingia katika siasa… lakini niliwahi kusema wakati wa kampeni kwamba
unaweza kumuondolea Rais Kikwete kila unachojisikia kumuondolea, lakini si utu. Rais Kikwete ana utu, ni mtu mwenye karama, unaweza kumkuta katika misiba hata ya watu wa kawaida sana.

“Hata nyie waandishi wa habari ni mashahidi… utamkuta Rais Kikwete hata katika msiba
wa mwandishi wa habari wa kawaida kabisa si mkurugenzi au kiongozi wa juu, la hasha.”

Anawataja pia Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib-Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed
Ali Shein, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Zanzibar,
Maalim Seif Shariff Hamad, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Spika wa
Bunge, Anne Makinda, mawaziri, naibu mawaziri na wabunge kuwa ni viongozi waliomfariji kila mara.

Kuhusu yaliyokuwa yakisemwa juu yake
Waziri Mwandosya alisema pamoja na ugonjwa, alikuwa anafuatilia kwa kina kile kinachozungumzwa na Watanzania wenzake kuhusu afya na ugonjwa wake.

Anautaja mtandao wa kijamii wa Jamii Forum kuwa ni moja ya vilivyokuwa vyanzo vyake vikubwa vya habari.

“Nilikuwa nasoma sana.. nilikuwa naona vijana wanabishana kuhusu afya yangu, wapo
waliokuwa wakiandika kuniombea nipate nafuu na nirudi nyumbani salama, lakini wapo
waliosema nifie kulekule India na mwili wangu urudi ukiwa kwenye sanduku (jeneza).

“Sikusikitishwa sana na maombi ya waliotaka nife maana nilifahamu hiyo pia ilikuwa ni
njia ya kuniombea uhai na miaka mingi zaidi duniani. Unajua unapozaliwa kutoka tumboni
mwa mama ni kitu kimoja tu ndio unakuwa na uhakika nacho, kwamba ipo siku utakufa. Hawa
niliona wanachokifanya ni kuniombea nitangulie tu lakini nilijua wao pia wanafahamu
kwamba watakufa.”

Kuhusu mgogoro wa afya yake kuhusishwa na masuala ya kisiasa, Waziri Mwandosya alipinga tetesi hizo. “Kuugua ni kitu cha asili. Nimesema sikuugua kwa miaka 34, kwa hiyo nilipougua sikuona kama ni jambo la kisiasa nilijua ni mipango ya Mungu na ni kitu cha asili.

“Wanasiasa tunaugua kama wanavyougua watu wengine. Ni kweli kwamba unapougua
unasikia mambo mengi na pia unapewa ushauri mwingi, wapo waliohusisha ugonjwa wangu na
mambo ya kisiasa, lakini wapo pia walionishauri nikitoka India nipite pia Nigeria… ni mambo
mazito maana usipoangalia unaweza kuzunguka Dunia nzima.

Kuwania urais mwaka 2015
Ingawa mwaka 2005, Profesa Mwandosya aligombea urais, alipotakiwa kuelezea msimamo wake kwa uchaguzi mkuu wa 2015, alisema ni mapema sana kuzungumzia uchaguzi huo wakati Serikali ya Kikwete inakabiliwa na kazi nzito ya kutekeleza ahadi ilizozitoa kwa wananchi.

“Kila kipindi cha utawala kina malengo yake ambayo kimewaahidi wananchi, unawaahidi
wananchi kwamba ndani ya miaka mitano tutatekeleza hili na lile.Serikali yetu imetoa ahadi
kubwa sana ingawa zinatekelezeka ndio maana tukazitoa. Mimi ni msimamizi wa sekta ya maji
ndani ya Serikali hii, sekta ambayo ina malengo mazito sana.

“Huu ni mwaka 2011, kwa hiyo ni mwaka mmoja tu tangu tulipotoa ahadi hizo kwa wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana 2010. Mwaka 2015 ndio tutakuwa tunakamilisha kipindi cha pili cha urais wa Rais Kikwete.

Hapa kuna mambo mawili, ama ushughulikie ahadi za wananchi au uanze kujipanga kugombea urais 2015. Kwangu jambo la msingi sasa ni kuwasaidia wananchi.

“Mwaka 2014 utakuwa mwaka muafaka kwangu kuulizwa suala la kuwania urais au la...Wapo wanaosema unapotaka urais unapaswa ujipange kwa miaka 10, lakini mimi najiuliza miaka 10 nitajipanga nini, hao wanaofanya hivyo wana fedha mimi sina fedha za kufanya hivyo bali ajenda yangu ni kuwatumikia wananchi.”

Atajiuzulu kutokana na afya yake?
Profesa Mwandosya alitupilia mbali hoja kwamba kazi ya uwaziri na ubunge ni nzito na
inayohitaji afya njema na kama ana mawazo ya kujiuzulu ili kupumzika na kuifanya afya yake
kuimarika zaidi.

“Kwanza kuna afya ya mwili kwa maana ya mfumo mzima wa mwili halafu kuna mambo
mengine kama afya ya kichwa kama kinaweza kufanya kazi ipasavyo. Yupo mwanasayansi wa
Marekani amepooza mwili wote na anashindwa hata kuzungumza.

Hata hivyo amewekewa mashine maalumu ambayo taya zake zinapojifungua kama kutaka kuzungumza jambo, mashine inaandika ni nini anataka kusema. Na leo hii ana mambo makubwa sana anaisaidia nchi yake… hilo ndio jibu langu kwa suala
hilo.”

Waziri Mwandosya alisema pamoja na kuulizwa sana ni ugonjwa upi unamsumbua alisema
hayupo tayari kuutaja kwa vile ni siri baina yake na daktari wake.

Alisema pamoja na afya yake kuimarika atarudi mara nyingine kwa daktari wake India ili kuendelea kuchunguzwa mwenendo wa uponaji wake.