Rais Jakaya Kikwete akitazama mandhari ya Jiji la Dar es Salaam kupitia kwenye mgahawa unaozunguka wa jengo la PSPF Golden Jubilee muda mfupi baada ya kuzindua jengo hilo lenye ghorofa 22 na urefu wa mita 100. (Picha na Fadhili Akida).

RAIS Jakaya Kikwete ameagiza wastaafu serikalini walipwe mafao yao siku wanapostaafu kwa kuwa hakuna sababu ya msingi ya kuwacheleweshea.

Katika kutekeleza hilo, ametaka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) kutumia
ofisi zake za Kanda kulipa wastaafu hao siku wanayostaafu.

Rais Kikwete alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua jengo la Makao Makuu ya PSPF na kusisitiza kuwa muda wa malipo ya mafao ya wastaafu wa mfuko huo ambao ni siku saba baada ya siku ya kustaafu bado ni mrefu.

Alisema yeye haoni sababu ya malipo hayo kucheleweshwa kwa kuwa mtumishi anapostaafu
huandika notisi ya miezi sita muda unaotosha kumuandalia mafao yake.

Rais Kikwete alisema ili kuepusha usumbufu, siku anapoagwa mstaafu na kwa kufanyiwa
sherehe, siku hiyo apewe mafao yake.

Aliwataka kuondokana na utaratibu wa sasa aliosema mfanyakazi anaagwa kwa sherehe
kubwa na kupatiwa vyeti, baada ya muda mfupi anaanza kusaga lami kufuatilia mafao yake.

Utaratibu huo kwa mujibu wa Rais Kikwete, unamfanya mstaafu kufuatilia mafao hayo kwa
gharama za kutoka mikoani na kurudi, jambo linalomlazimu kukopa fedha hizo pamoja na za
matumizi akifuatilia mafao yake.

Kikwete alisema jambo la kushangaza ni kukuta hali ya kusumbuliwa kuwa taarifa zake
hazionekani au mara nyingine akitakiwa kupeleka barua ya kuajiriwa.



“Utakuta mtu kaajiriwa, ana miaka arobaini au hamsini huku akihama kutoka mkoa mmoja
hadi mwingine na barua kaipoteza, sasa mnamlazimisha kupeleka barua wakati taarifa
zote za wafanyakazi zipo serikalini?” alihoji.

Alisema usumbufu huo mara nyingi ndiyo chanzo cha rushwa na kukemea kuwa siyo jambo
zuri na linawezekana kuondolewa.

“Hili, Yambesi (Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George)
linakuhusu wewe na ofisi zote za Serikali kujua muda wa kustaafu kwa wafanyakazi na kuwapa
hundi siku ile ya sherehe ya kustaafu,“ alisema.

Rais alitaka watendaji Serikalini wanaokwamisha utoaji wa mafao hayo kwa wakati kutovumiliwa wala kuwaonea huruma kwa kuwa ni wanyanyasaji wa wastaafu na kuagiza wachukuliwe hatua.

“Wahurumieni hawa watu wazima waliochoka kwa kuzifanya ofisi za kanda zimalizane
nao kila kitu na shabaha yenu iwe wakati anaondoka, apate kila kitu chake, fedha zake za likizo,
nauli na madai yake yote,” alisema.

Alisema baada ya malipo hayo, matumizi ni juu yake, kama atanywea pombe au kuongeza mke hiyo ni juu yake lakini jambo la msingi amelipwa fedha zake zote na kubaki kupata zile za mwezi ambazo zimepangiwa utaratibu maalumu.

Mikopo kwa wafanyakazi
Rais pia aliutaka mfuko huo kuwa na miradi mingi inayomnufaisha mwanachama moja kwa
moja kwa kutoa mikopo ya kuwajengea wanachama wake nyumba za bei nafuu kabla ya
kustaafu, ili kuongeza ufanisi sehemu za kazi.

“Unajua mfanyakazi akiwa na nyumba kuna utulivu kazini, kaeni na Hazina muone namna ya kutumia mfuko wa mikopo ya nyumba na nyie mkiongeza kidogo muwapatie mikopo hiyo
wanachama wenu,” alisema.

*Miradi isiyo na tija
Pia aliitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuendelea kuwekeza katika miradi yenye faida na tija
kwa mfuko huku ikiwanufaisha wanachama.

“Siyo kwamba mzee kasema anzisheni mradi fulani mnafuata, fanyeni uamuzi wa tija isiwe
mnafanya miradi kwa kuwa mzee kasema,“ alisema.

Aliwataka wafanye utafiti na uchunguzi wa kutosha na kama wakigundua mradi haufai na
mzee analazimisha, wamwambie haiwezekani kwa kuwa atafoka tu na wao watakuwa wameokoa mfuko.

“Mkiona mzee anawalazimisha sana, niambieni kwani mimi ndiyo mkubwa wao wote,
msikubali miradi kirahisi ndiyo maana mkinieleza mnataka kuanzisha mradi nawahoji sana,”
alisema.

Aliwataka kutambua kuwa wanawajibika kwa wanachama wanaokatwa fedha zao na siyo kwa wazee wanaotoa maagizo.

Awali, akimkaribisha Rais kuzindua jengo hilo, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo alisema sekta ya hifadhi za jamii inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo utaratibu wa kisheria uliopo ambao mifuko ya pensheni husimamiwa na wizara tofauti badala ya kuwa chini ya wizara moja.

Changamoto nyingine ni ya wigo finyu wa wateja, ambao ni asilimia 2.5 tu ya Watanzania na
tofauti kwenye ukokotoaji wa mafao kati ya mifuko iliyopo.