RAIS DKT. JAKAYA KIKWETE AKIWASILI KWENYE UWANJA WA NDEGE WA ENTEBBE NCHINI UGANDA TAYARI KUHUDHURIA MKUTANO WA NCHI ZA MAZIWA MAKUU KUPINGA UNYANYASAJI NA UKATILI WA KIJINSIA.
RAIS DKT. JAKAYA KIKWETE AKIONGEA NA RAIS WA ZAMBIA NA MWENYEKITI WA ICGLR ALIYEMALIZA MUDA WAKE,MH MICHAEL CHILUFYA SATA (KUSHOTO) NA RAIS MWAI KIBAKI WA KENYA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA NCHI ZA MAZIWA MAKUU KUPINGA UNYANYASAJI NA UKATILI WA KIJINSIA.

Rais Kikwete na ujumbe wake amewasili nchini Uganda asubuhi ya leo na kwenda moja kwa moja kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili.
Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi wa mkutano huo ni pamoja na Rais Michael Chifunya Sata wa Zambia ambaye amemaliza muda wake wa kuwa mwenyekiti wa ICGLR na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, mwenyeji wa mkutano huo na mwenyekiti mpya wa Umoja huo.
Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Rais Mwai Kibaki wa Kenya na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi. Nchi nyingine wanachama wa ICGLR zilizowakilishwa na viongozi wa ngazi mbali mbali ni Sudan ambayo imewakilishwa na Makamu wa Rais Dkt. Alhaj Adam Yusuf, Angola, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Congo Brazzaville na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
Katika siku ya kwanza ya mkutano huo leo, viongozi na wawakilishi wa nchi wanachama wa ICGLR wamejadili suala zima la Ukatili wa Kijinsia na athari zake katika nchi za Maziwa Makuu ambako kumekuwa na aina moja ya vita na mapigano kwa miaka 17 iliyopita.
Ukatili wa Kijinsia katika nchi ambazo zinakabiliwa na mapigano na vita ama zimetoka katika hali hiyo unachukuliwa kuwa ni pamoja na ubakaji, mashambulizi wa kijinsia, kupiga, utekaji nyara, mauaji ya makusudi, utumwa wa kijinsia, ndoa za kulazimishwa na kufanya mapenzi na watoto wadogo.
Kesho, mkutano huo utajadili masuala mengine yanayohusiana na Umoja huo ikiwa ni pamoja na kujadili hali ya usalama katika nchi wanachama wa ICGLR, na kupokea na kujadili ripoti ya mkutano wa mawaziri wa usalama na ulinzi kuhusu athari za majeshi hasi katika eneo hilo.

Mkutano huo pia utajadili na kutoa uamuzi kuhusu maombi ya nchi za Sudan Kusini kujiunga na ICGLR.
Mkutano huo wa mwaka huu pia utajadili maendeleo yaliyopatikana kutokana na maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano maalum wa ICGLR uliofanyika Lusaka, Zambia mwaka jana kuhusu mapambano dhidi ya uvunaji na biashara haramu ya maliasili za nchi hizo.
Katika kikao hicho, wakuu hao wa nchi pia watateua Katibu Mtendaji mpya wa ICGLR kufuatia kumalizika kwa kipindi cha uongozi cha Balozi Liberata Mulamula wa Tanzania.
Muhula wa uongozi wa Balozi Mulamula ulimalizika tokea mwaka jana wakati wa mkutano wa Lusaka, lakini wakuu wa nchi wanachama wa ICGLR walimwomba balozi huyo wa Tanzania kuendelea kushikilia nafasi hiyo kwa mwaka mmoja zaidi ili kutoa nafasi kwa nchi wanachama kutafuta watu wanaofaa kujaza nafasi hiyo.

IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULUDESEMBA 15, 2011KAMPALA