NA IMELDA MTEMA
ILE muvi ya mume wa Irene Uwoya, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ kutorokea kusikojulikana na mtoto wao kipenzi, Krish, linaendelea ambapo kipande (scene) hiki kinaonesha kuwa mwanaume huyo amemtumia mkewe meseji ‘SMS’ ya kifo.
TUJIKUMBUSHE
Habari ya kutoweka kwa Ndikumana na mtoto iliyoripotiwa kwa mara ya kwanza na gazeti tumbo moja na hili, Ijumaa Wikienda, Jumatatu wiki hii, likieleza kuwa Alhamisi iliyopita Ndikumana aliondoka nyumbani kwake, Sinza, Dar es Salaam na kwenda kwa mama wa Uwoya, Mbezi-Jogoo ambapo alimchukua mtoto huyo na mwingine ambaye ni wa kwake, aitwaye Baset kisha kutokomea.

AMWAMBIA UWOYA AJIANDAE KUITIWA MAITI TATU
Akizungumza na 5 Star Paper, Risasi Mchanganyiko, Uwoya alifunguka kuwa wakati akihaha kumpata mwanaye, aliishiwa nguvu alipopokea SMS kupitia kilongalonga cha kiganjani iliyotumwa na Ndikumana ikimweleza kwamba ajiandae kuitiwa maiti tatu.

Aliposema maiti tatu alimaanisha moja ya kwake (Ndikumana), ya pili ya mtoto wao na ya tatu ni ya yule mtoto mwingine wa Ndikumana (Baset).
UWOYA LAIVU
“Kiukweli simwelewi Ndikumana hata kidogo, kwa nini anitumie meseji ya aina hii ukizingatia yeye ndiye katoroka na mtoto?”

AKOSA USINGIZI
 “Napata wakati mgumu sana katika maisha yangu, hapa nilipo presha tupu. Ndikumana ameninyima usingizi, silali namuwaza mtoto wangu, amenisikitisha sana, siwezi kuvumilia, lazima nimchukulie hatua za kisheria.”


NI KITENDO CHA KINYAMA
Uwoya aliendelea kutambaa na mistari kuwa kitendo alichokifanya Ndikumana ni cha kinyama kwa sababu bado mtoto ni mdogo na anahitaji uangalizi wa karibu wa mama (yeye).

KUMBE KUNA UGOMVI!
“Najua mwanangu anateseka sana bila hatia. Hata kama tuna ugomvi, haimhusu mtoto hata kidogo.”
Uwoya alipotakiwa kueleza wana ugomvi gani na mumewe, hakusema chochote kwa maelezo kwamba ni mambo ya kifamilia zaidi.

UJUMBE WA MAUAJI WAMCHANGANYA
Uwoya ambaye ni moto wa kuotea mbali katika muvi za Kibongo, alikiri kuwa ujumbe wa mauaji aliotumiwa na Ndikumana umesababisha aongeze jitihada za kumsaka popote alipo kwa msaada wa jeshi la polisi na atakapompata atakuwa na kesi ya kujibu.

NDIKUMANA VIPI?
Kama ilivyo desturi ya magazeti ya Global Publishers kutafuta mzani wa habari, gazeti hili lilitumia muda mwingi kumpigia na kumtumia SMS Ndikumana, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba kufuatia simu yake kutokuwa hewani.

Subira iliendelea, likiamini kwamba baada ya kupokea SMS yake, angelipigia lakini mpaka tunakwenda mtamboni, SMS zote zilitumwa kwa Ndikumana, zilionekana zipo ‘pending’
NYUMA YA PAZIA
Habari za chini kwa chini zinadai kuwa tangu ndoa ya wawili hao ilipopigwa na kimbunga hivi karibuni, mambo hayajatulia, huku maneno yakienea kwamba bado Ndikumana ana kinyongo hivyo analipa kisasi.

NDIKUMANA AJISALIMISHA
Juzi, Jumatatu mishale ya saa 10:48 za jioni wakati gazeti hili likijiandaa kwenda mitamboni, zilitua habari kwamba, Ndikumana amemrudisha mtoto huyo.