Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Iringa, imesema inapoteza zaidi ya Sh. milioni 11 kila mwaka kutokana na kukithiri kwa biashara ya magari madogo ya kukodi maarufu kama teksi bubu kwa kukwepa kulipa ushuru wa maegesho.
Magari hayo yanayodaiwa kuwa zaidi ya 100 katika Manispaa ya Iringa yanadaiwa kutumia mbinu mbalimbali kukwepa kusajiliwa na serikali katika biashara ya teksi.
Meneja wa TRA Mkoani hapa, Rosalia Mwenda alisema kuwa Mamlaka hiyo imeanza operesheni maalumu ya kusaka magari hayo kwa lengo la kuyakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaofanya udanganyifu huo.
“Tumeanza operesheni maalumu dhidi ya wamiliki wa teksi bubu ambazo zinafanya kazi katika Manispaa ya Iringa na kila atakayekamatwa atachukuliwa hatua kali ikiwemo kufikishwa mahakamani,” alisema Mwenda. Meneja huyo alifafanua kuwa hadi kufikia sasa, TRA mkoani hapa inaendelea kufuatilia madeni yake ambayo hayajalipwa na wafanyabiashara zaidi ya Sh. bilioni 1.
Vilevile alisema TRA imepata hasara ya zaidi ya Sh. milioni 130 kwa madeni yasiyolipika kutokana na wengi wa wafanyabiashara kufariki dunia na wengine kuhamisha biashara zao kwa lengo la kukwepa kulipa kodi ya serikali.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato yake katika mwaka wa fedha 2011/12, Mwenda, alisema TRA Iringa imepangiwa kukusanya kiasi cha Sh. 23,7761,800.(picha haihusiani na habari,picha kutoka maktaba)