Maelfu ya waandamanaji katika sehemu mbalimbali za Urusi, wanataka uchaguzi wa bunge uliofanywa Jumapili iliyopita, urejelewe.
Maandamano makubwa kabisa yamefanywa mjini Moscow, ambako mwandishi wa BBC, anasema maelfu ya watu wako katika medani, ng'ambo ya pili ya mto, mkabala na ofisi za serikali.
Akihutubia watu wanaopepea bendera, Waziri Mkuu wa zamani wa Urusi, Mikhail Kasyanov, alisema watu wamechoka kufanywa kama ng'ombe.
Maandamano mengine madogo yanafanywa sehemu nyengine za Urusi, pamoja na St Petersburg, ambako kulitokea msukumano kati ya polisi na waandamanaji.
Waandamanaji wanasema kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita, ambapo chama tawala cha United Russia kiliongoza.