Wapatanishi wameingilia kati kuzuia vurugu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kabla ya kutolewa kwa matokeo kamili ya uchaguzi.
Wanaowaunga mkono wapinzani wameonya kuwa wataukataa ushindi wa rais Joseph Kabila, kwa madai kumefanyika wizi mwingi wa kura.
 
Ikiwa takriban aslimia 90 ya kura zimehesabiwa kutoka uchaguzi wa Jumatatu iliyopita, Bw Kabila ana aslimia 49, dhidi ya asilimia 33 za mpinzani wake mkuu, Etienne Tshisekedi, kulingana na matokeo rasmi.
Polisi maalum wa kuzuia ghasia wamekuwa wakifanya doria kwenye mji mkuu, Kinshasa.
Mabomu ya kutoa machozi yametumika kuwasambaza wafuasi wa Bw Tshisekedi katika matukio mbalimbali wiki hii kwenye mji mkuu huo, unaoonekana kuwa ngome ya wapinzani.
Uchaguzi uliopita, mwaka 2006, uligubikwa na ghasia mitaani iliyoongozwa na wafuasi wa mgombea aliyeshindwa, Jean-Pierre Bemba.
Kwa sasa ana kesi katika mahakama ya kimataifa kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita kwenye nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

'Heshimu matokeo'

DRC, nchi yenye ukubwa wa theluthi tatu zaidi ya Ulaya Magharibi na amabyo haina barabara za lami au miundo mbinu mingine, inajitahidi kurejesha hali yake kutokana na vita vya mwaka 1998-2003 viliyosababisha vifo vya takriban watu milioni nne.
Kundi la wapatanishi-lililoundwa kwa kusaidiwa na tume ya uchaguzi na ujumbe wa umoja wa mataifa huko Kongo- limefanya mazungumzo na Bw Kabila na Bw Tshisekedi kwa nia ya kupunguza wasiwasi, mwenyekiti wake, Sheikh Abdallah Mangala, kiongozi wa dini ya kiislamu, ameiambia BBC.
Alisema, "Kila mmoja ataheshimu matokeo yatakayotoka kwenye sanduku la kupigia kura".
Hata hivyo, Bw Tshisekedi aliweka masharti kwamba tume ya uchaguzi lazima ichapishe taarifa zote kutoka kila kituo cha kupigia kura, zikiwemo idadi ya kura ambazo kila mgombea kapata, alisema Bw Mangala, akiongeza kuwa tume ilikubaliana na hilo.
Kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, ghasia za uchaguzi tayari zimesababisha vifo vya takriban watu 18 na zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Tume hiyo ilisema itachapisha matokeo yote ya majimbo siku ya Alhamis, baada ya kuchelewa kwa saa 48 kutokana na matatizo ya kukosa vifaa.
Imetoa lawama vya vifo hivyo zaidi kwa walinzi wa rais, likiwashutumu kuwapiga risasi wafuasi wa upinzani- mashtaka amabayo serikali imeyakana.
Mbali na uchaguzi wa rais, zaidi ya wagombea 18,000 wanachuana kwa nafasi 500 za ubunge.
Bw Kabila, mwenye umri wa miaka 40, amepata upinzani mkubwa kutoka kwa Bw Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 78, na wagombea wengine tisa.

                                              CHANZO CHA HABARI