WAUGUZI wakunga vituo vya Afya katika Manispaa ya Morogoro, wanalazimika kutumia tochi za simu za mkononi, kandili na mishumaa kuweza kuwasaidia akina mama wajawazito kujifungua.

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti na Waganga Wafawidhi wa Vituo vya Afya vya Mafiga, Sabasaba na Kingolwira , vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro, wakati wa ziara maalumu ya Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, ya kuvitembelea vituo hivyo pamoja na zahanati zinazomilikiwa na Manispaa.


Wauguzi wakunga hao wamesema kwamba wanalazimika kutumia mfumo huo wa kupata mwanga kwa kuwa pamoja na kuwa na majenereta ili yatumike pindi umeme unapokatika, tatizo kubwa ni mafuta.


Mbali na tatizo hilo vituo hivyo vinakabiliwa na upungufu wa watumishi wakiwemo madaktari sanjari na vifaa tiba ambavyo ni nyuzi za kushonea msamba, vitanda vya kuzalishia, mashuka na mablanketi ya kujifunika wanawake baada ya kujifungua.


Ziara hiyo maalumu ya Mbunge huyo iliyofanyika juzi kusikiliza kero za wagonjwa na matatizo yanayovikabili Vituo vya Afya na Zahanati na kuangalia namna ya kuyatatua kwa kushirikiana na Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa.



Akizungumzia tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme na ukosefu wa mafuta unaojitokeza katika Kituo cha Afya Mafiga, ambacho kimeteuliwa kuwa ni cha kujifungulia akinamama pamoja na huduma nyingine, Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Dk. Benny Ngereza, alisema kituo kinakabiliwa na matatizo mengi.


Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi huyo, wanawake wanaojifungulia kwenye Kituo cha Afya Mafiga ni kati ya 450 hadi 600 kwa mwezi na hivyo kituo huelemewa; hasa kutokana na ufinyu wa wadi ya akinamama, vifaa tiba ikiwemo na mipira ya kuzalishia, ukosefu wa mara kwa mara wa mafuta ya gari la wagonjwa na jenereta.


“Tumetakiwa tutumie fedha za mfuko wa makusanyo ya kituo kwa ajili ya kununua mafuta, lakini fedha za Kituo hazitoshelezi kwa vile upande wa akinamama wajawazito na watoto hawatozwi fedha” alisema Dk. Ngereza.


Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa wadi ya kuzalia akinamama Dk. Magdalena Kongera, chumba cha kuzalia kina upungufu wa vitanda ambao kwa sasa ni kitanda kimoja ndicho kinachotumika baada ya kingine kuwa kibovu na ili kukidhi mahitaji vinahitajika vitanda vitatu.


“Chumba hiki cha kuzalishia akina mama kina uhaba wa vitendea kazi vingi , kukosekana kwa umeme mara kwa mara, na jenereta mara nyingi linakosa mafuta, inapotokea hali hii na kuna mzazi wa kumzalisha tunalazimika kutumia vibatari ama taa za simu zetu …ambapo kwa siku tunazalisha akinamama 15 hadi 20 ambao wanatoka kata mbalimbali za Manispaa “ alisema Dk. Kongera.


Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo hilo akiwa kwenye Kituo cha Afya Nunge, alifahamishwa na Mganga Mfawidhi , Dk. Oresta Mwambe, kuwa kituo kinakabiliwa na wingi wa wagonjwa wanaokadiriwa 100 hadi 150 kwa siku wanaotoka kata mbalimbali za manispaa hiyo.


Hata hivyo alisema kituo hicho kina upungufu wa madaktari na waliopo ni sita wakati wanahitajika kumi na kushauri Halmashauri ya Manispaa iharakishe kufungua Zahanati ya Kata ya Mwembesongo ili kupunguza wingi wa wagonjwa wanaotoka kwenye eneo hilo.


Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sabasaba, Dk. Perepetua Dumyeko, alisema pamoja na kutoa huduma za afya, kituo kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi, vyumba vya kutolea huduma , ukosefu wa choo katika kitengo cha VVU , ufinyu wa chumba cha maabara na vyumba vya kupima kifua kikuu na Virusi vya Ukimwi.


Pamoja na hayo alisema, umeme unapokatika huduma zote za maabara, ung’oaji wa meno zinasimama kwa kuwa kituo hicho hakina jenereta, kituo kukosa ulinzi nyakati za mchana na uhaba wa maji.


Kilio kama hicho pia kimekikumba Kituo cha Afya Kingolwira, kinachohudumia zaidi ya wananchi 13,000 wa kutoka kata hiyo na nyingine za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.


Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Dk. Thobias Fimbo, alisema Kituo kinakabiliwa na uhaba wa dawa na mara nyingine zinapoagizwa zinakosekana kuletwa hasa dawa za Alu ‘ Dawa Mseto’ za kutibu ugonjwa wa malaria.


Pamoja na hayo alisema, kituo hicho hakina jenereta na umeme ni wa matatizo, hivyo wakunga wauguzi wanalazimika kutumia vibatari wakati wa kutoa huduma za kuzalisha jambo ambalo ni la hatari , ikiwa na ukosefu wa gari la wagonjwa.


Akitolea ufafanuzi wa baadhi ya changamoto zinavikabili vituo vya Afya na zahanati za Manispaa ya Morogoro, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dk. Abraham Mahizo, pamoja na kukiri kuwepo kwa uhaba wa vitendea kazi , alisema vituo hivyo vinategemea bajeti ya Halmashauri.


Akizungumzia matatizo ya Kituo cha Afya Mafiga ambacho kimeteuliwa kutoa huduma za kuzalisha akina mama wajawazito, alisema licha ya Hospitali ya Mkoa kuteua kufanya kazi hiyo, bado hakipati ruzuku ya kuwahudumia.