Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas), kimewasimamisha masomo kwa muda usiojulikana wanafunzi 66 walioshiriki kwenye vurugu chuoni hapo Desemba 8 na 10, mwaka huu kutokana na vurugu.
Uamuzi huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kisali Pallangyo, alipozungumza na waandishi wa habari.
Profesa Pallangyo alisema kati ya wanafunzi hao waliosimamishwa, mmoja ni mwanamke na 65 ni wanaume.
Wakati wanafunzi hao wakisimamishwa masomo kwa muda usiojulikana, chuo hicho kimesema kuna taarifa kwamba kuna vurugu zinaandaliwa tena ambazo zitafanyika Desemba 19, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Profesa Pallangyo, chuo kina taarifa za uhakika kwamba wanafunzi wameandaa vurugu nyingine siku hiyo ambapo alisema wameishavijulisha vikosi vya usalama kwa ajili ya kuweka ulinzi.
Wanafunzi waliosimamishwa masomo wengi wao ni wale wa mwaka wa tatu na wa tano na kwamba tayari uongozi wa chuo umeishawaandikia barua rasmi za kuwasimamisha.
Hata hivyo, Profesa Pallangyo alisema kila mwanafunzi aliyesimamishwa masomo atatendewa haki na kwamba hakuna mtu atakayeonewa na chuo.
Alisema vurugu za kwanza zilifanyika chuoni hapo Desemba 8, siku ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa ajili ya kuonyesha tafiti ambapo wanafunzi hao walivuruga sherehe hizo na kumzingira Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, ambaye alikuwa mgeni rasmi pamoja na ujumbe wake.


Aidha, Profesa Pallangyo alisema Desemba 10, mwaka huu, siku ya mahafali, wanafunzi hao tena walirudia vurugu hizo ambapo walitaka kuvuruga sherehe hizo, lakini wakatawanywa na vikosi vya usalama.
Vitendo vya uvunjifu wa amani viliendelea kufanywa na wanafunzi hao kati ya Desemba 12 na 13, mwaka huu, ambapo Desemba 14, mwaka huu, Baraza la Chuo lilikutana kwa dharura na kujadili vurugu hizo na kufikia maamuzi ya kuwasimamisha wanafunzi hao masomo.
Alisema madai ya msingi ya wanafunzi hao ni kutaka kurudishwa kwa serikali ya wanafunzi chuoni hapo (Muhasso), ambayo ilifutwa na Baraza la chuo hicho.
Wanafunzi hao pia wanataka Profesa Pallangyo kuondolewa katika nafasi hiyo, madai ambayo yeye mwenyewe jana aliyapinga na kusema kuwa tatizo sio yeye kwani amefanya mambo mengi yanayohusiana na maendeleo ya chuo.
“Mimi sio tatizo, hata hivyo, mimi nasimamiwa na mamlaka zilizo juu yangu na hizo ndizo zitakazopima kama nastahili kuwepo ama kuondolewa,” alisema Profesa Pallangyo.
Alisema vurugu za wanafunzi hao zinatokana na serikali kutaka Muhasso ifanye marekebisho katika katiba yake kama ilivyoagiza kwenye vyuo vikuu vingine, lakini wao wakakaidi agizo hilo halali.
Hata hivyo, Muhasso baada ya kukataa agizo hilo la serikali iliomba kukutana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kumueleza kilio chao, ingawa pia hawakufikia mwafaka.
Kutokana na misuguano hiyo, Baraza la chuo hicho liliamua kuifuta Muhasso mpaka hapo sheria ya GN 178 iliyotolewa na serikali itakapofanyiwa kazi.
Chuo hicho kimesema baada ya wanafunzi hao kusimamishwa masomo, wataitwa mmoja mmoja na kumpa nafasi ya kujieleza na kwamba wale watakaopatikana na hatia ya kuongoza vurugu hizo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Wakati Muhas kikiwasimamisha wanafunzi hao, juzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kiliwafukuza wanafunzi wake 43 na kutaka wasisajiliwe katika chuo chochote hapa nchini kwa ajili ya masomo.
Wanafunzi hao walifukuzwa na Baraza la Chuo kutokana na kuhusishwa na vurugu kubwa za Desemba 12 na 13, mwaka huu.