Wanajeshi wa mwisho wa Marekani nchini Iraq sasa wameshaondoka kabla ya siku ya mwisho wa mwaka, ambao ndio wakati uliokubaliwa baina ya Iraq na Marekani.
Gari la jeshi la mwisho lilivuka mpaka na kuingia Kuwait asubuhi mapema, na kumaliza vita vya Iraq vya karibu miaka 9, muda mrefu kushinda ilivotarajiwa awali.
Msafara wa mwisho wa matingatinga kama 110 uliwasili Kuwait, ukishangiliwa, na wanajeshi kukumbatiana.
Msafara huo ulikuwa na wanajeshi 500 wa mwisho wa Marekani kuondoka Iraq.
Katika vita vya Iraq Marekani ilipoteza karibu wanajeshi 4500 na zaidi ya 30,000 walijeruhiwa.
Inakisiwa raia zaidi ya laki moja wa Iraq waliuwawa, na haijulikani wangapi wameachwa na vilema katika mitibuko ya nchi hiyo.

Sasa Wamarekani wanaondoka, lakini Marekani itaendelea kuwa na madaraka kupitia ubalozi mkubwa ambao utakuwa piya na maafisa wa kijeshi 150 wataoshughulikia biashara ya silaha kwa Iraq; pamoja na raia mia kadha wa kuwafunza wanajeshi wa Iraq namna ya kutumia vifaa vya Marekani.