Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka(Pichani kushoto), amewarejeshea wamiliki halali nyumba ya Wakfu wa Msikiti iliyoporwa na wajanja wachache kwa miaka 21 iliyopita, huku akiwataka watu wanaojimilikisha nyumba na viwanja kwa njia za utapeli, kuacha tabia hiyo mara moja, vinginevyo watashughulikiwa bila kuangaliwa usoni.
Nyumba hiyo ambayo ilitolewa Wakfu na marehemu Hajati Aziza Omar kwa Msikiti wa Mwinyi, ulioko Ilala, iko kwenye Kitalu namba 77, Kiwanja namba 32, Mtaa wa Somali, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Profesa Tibaijuka alitoa onyo hilo wakati akikabidhi hati ya kiwanja cha nyumba hiyo kwa wadhamini wa msikiti huo jijini Dar es Salaam jana, ambao walisaini hati hiyo mbele yake katika hafla fupi ya makabidhiano ya hati hiyo.
Alisema matatizo ya watu kujimilikisha nyumba na viwanja kwa njia za utapeli, yamekuwa mengi nchini na kwamba, aliyejimilikisha kiwanja cha nyumba hiyo, alitumia mwanya huo kutokana na ucheleweshaji wa umilikishaji.

Aliwataka viongozi wa dini kuwa macho na kulinda mali za misikiti na makanisa dhidi ya uporaji unaoweza kufanywa na matapeli hao.
“Tusipokuwa macho, watu hao watajimilikisha, kwani tatizo hili haliko hapa tu, lipo sehemu nyingi,” alisema Profesa Tibaijuka, ambaye katika hafla ya makabidhiano ya hati hiyo jana, aliongozana na Kamishna wa Ardhi, Anna Mdemu na Msajili wa Hati, Subira Sinda kutoka wizara hiyo.
Aliongeza: “Watu hao kama wapo waache. Mchezo umekwisha. Wizarani hatuangalii usoni, tunaangalia haki.”
Kabla ya kuhutubia na baadaye kukabidhi hati hiyo, Profesa Tibaijuka, aliwaomba viongozi wa Kiislamu, waumini na watu wote waliohudhuria hafla hiyo, kusimama kwa dakika moja kumkumbuka marehemu Hajat Aziza aliyetoa nyumba hiyo itumike kwa maslahi ya msikiti huo. Awali, Imamu Mkuu wa Msikiti huo, Sheikh Abeid Maulid, alisema kiwanja cha nyumba hiyo kiliporwa mwaka 1991 ikiwa ni siku chache baada ya Hajat Aziza kufariki dunia.
Alisema baada ya hapo walianza jitihada mbalimbali kukomboa kiwanja hicho, ikiwa ni pamoja na suala hilo kulifikisha kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye aliwarudisha kwa Profesa Tibaijuka.
Sheikh Abeid alisema wanamshukuru Profesa Tibaijuka kwa ukarimu na uadilifu wake uliowezesha kurejeshewa nyumba hiyo.
Naye Imamu Mkuu wa Msikiti wa Idrisa, ulioko Kariakoo, Maalim Ali Bassaleh, alisema tatizo hilo lisingetokea kama Waislamu wangekuwa na Mahakama ya Kadhi, ambayo hushughulikia pia masuala ya Wakfu.