MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema,pichani) amewataka wabunge waliopokea posho mpya warejeshe katika akaunti ya Bunge kiasi kilichoongezwa kwa sababu kimetolewa kinyume cha sheria.

Alisema hayo jana katika tafrija ya miaka 50 ya ushirikiano wa Shirika la Uingereza la Maendeleo Kupitia Shughuli za Kujitolea (VSO) na Tanzania iliyofanyika Dar es Salaam kama
sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yanayofikia kilele leo.

“Nitasimama kidete kuhakikisha posho zilizoongezwa zinarejeshwa katika akaunti ya Bunge ili kulinda maslahi ya umma.

“Wote waliozipokea wamevunja Sheria ya Utawala wa Bunge ya mwaka 2008, kifungu cha 17 inayotaka malipo ya posho zote yatolewe kwa maandishi na kusainiwa (kuidhinishwa) na Rais.
Wanapaswa kuzirudisha na kuonesha stakabadhi kuwa wamefanya hivyo.”

“Huo ndio ukweli kwa sababu Rais hajaziidhinisha. Bunge ndio linalotunga sheria hivyo halipaswi kuwa kiongozi wa kuzivunja,” alisema.

Alisema kuwa wabunge hawana budi kuchagua moja kati ya mshahara na posho, vinginevyo watakuwa wanaendekeza maslahi binafsi tofauti na ilivyokuwa wakati nchi ilivyopata Uhuru ambapo wawakilishi wa wananchi walilipwa posho bila mshahara na kutekeleza majukumu yao
ipasavyo.

Alisema kikao cha wabunge cha mwaka 1978 Chake Chake, Zanzibar kilipitisha mshahara na kufuta posho baadaye mwaka 1985.

“Sasa mambo yaligeuka baada ya kuanza kwa vyama vingi ambapo posho zilianza kutolewa sambamba na mshahara lakini sheria haielekezi hivyo,” alisema.

“Ndio maana sisaini mahudhurio. Sitaki kuingiziwa posho kwenye akaunti na kujitetea kuwa ziliingizwa automatically kwenye akaunti. “Wote wanaozipokea na kujitetea kuwa wanazipokea kwa kuwa wanazikuta kwenye akaunti wanazipenda na kuzitaka kwa sababu
wanafahamu utaratibu kuwa ukisaini unawekewa,” alisema Zitto.





Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema, “Kama Ikulu wamesema hawajaidhinisha kweli na sio maneno tu ya waandishi basi itakuwa ni makosa kuzipokea kwa sababu hiyo ndiyo ofisi yenye mamlaka ya kisheria ya kuzihalalisha au kuzibatilisha.”

“Ndio maana nikasema Ikulu ndio wenye neno la mwisho, wakisema hazijasainiwa acheni kupokea tutafanya hivyo ingawa ninaelewa pia kuwa Tume ya Huduma za Bunge ndio mwajiri wa wabunge anayeshughulikia malipo yao na kumshauri Rais,” alisema ndugai.

Alikumbusha kuwa posho hutolewa endapo Rais ameshauriana na Tume hiyo inayotaka posho
ziongezwe kwa maoni kuwa za awali ni kidogo, na kuongeza; “Zitto hahusiki kabisa na masuala ya posho anapaswa akasimamie shughuli za maendeleo jimboni mwake.”

Sambamba na hilo pia alisema kuwa Spika wa Bunge, hufanya uamuzi kwa kuzingatia sheria inayoruhusu maoni ya wengi kupewa ushindi ndio maana msimamo wake katika suala la posho ni kuwa ziendelee kutolewa kwa sababu wengi wamezikubali.

Makinda alikiri nyongeza ya Sh 130,000 na kufanya posho mpya kuwa Sh 200,000 Dar es Salaam siku tano zilizopita, baada ya kuzindua ripoti ya Maendeleo ya Wanawake Duniani
katika kufikia haki kwa mwaka 2011.
                                               CHANZO CHA HABARI