Mohamed Mursi
Mohammed Mursi ametangazwa mshindi katika uchaguzi wa Rais nchini Misri.
Mursi ameshinda kura kwa asili mia 51.7% akimshinda mpinzani wake wa karibu Ahmed Shafik kwa mujibu wa tangazo la tume ya uchaguzi wa juu wa Rais.
Mkuu wa jopo la Majaji, Farouq Sultan, amesema kua wamezingatia malalamiko 466 kutoka kwa wagombea, ingawa matokeo ya uchaguzi hayatobalika.
Wafuasi washangilia Cairo
Tangazo hilo lilifuatiwa na shangwe na vigelegele katikakati ya medani ya Tahrir mjini Cairo ambako wafuasi wengi wa Bw.Mursi walikua wamekuanyika.

Wafuasi hao wamekaa kwenye medani hio kwa siku kadhaa wakionyesha msimamo wao wa kuchukia sheria kadhaa zilizotangazwa na Baraza la juu la utawala wa majeshi ambayo wanadai zimeundwa ili kupunguza mamlaka ya Rais na kuelekeza uwezo mkubwa kwa majeshi.


Wafuasi wa Bw.Shafiq nao waliweka kambi yao katika eneo la kaskazini mwa mji ambako kuna makao makuu ya Tume ya uchaguzi huko Nasser City.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi Jaji Sultan alianza kwa kunena kua tangazo la matokeo ya uchaguzi yalikua yamezongwa na shinikizo pamoja na hali ya wasiwasi.
Tume ya uchaguzi ilizingatia sheria ilipochunguza visanduku vya kupigia kura, na Jaji.Sultan alisema hakuna kilicho juu ya sheria.

Jaji huyo akaongezea kukanusha madai mawili nyeti kuhusu njama za kuibia uchaguzi, kwamba baadhi ya karatasi za kupigia kura ziliwekwa ndani ya visanduku tayari zikiwa na majina ya mgombea wanayemtaka ashinde.

Hatimaye Jaji Sultan akamtangaza mshindi kua ni Bw.Mursi ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha Muslim Brotherhood cha Freedom and Justice, Bw.Mursi.

Baada ya dakika kadhaa akitangaza marekebisho kuhusu matokeo madomadogo ya kura ndipo akamtangaza Bw.Mursi kua mshindi kwa kuzoa kura 13,230,131, na Bw.Shafiq akiweza kuzoa 12,347,380, sawa na asili mia 48.27%.