Stori: George Kayala
SAGA la mwigizaji wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel (pichani) kuvaa nusu utupu na kukaa kihasara huku maungo nyeti yakichungulia, limechukua sura mpya baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kumjia juu, Ijumaa Wikienda linafunguka.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego, wasanii wamekuwa wakionywa mara kwa mara kuhusu kuzingatia maadili na kuacha kuvaa nguo za nusu uchi hivyo inapotokea mmoja wao akawa kichwa ngumu, basi huyo atakuwa na ugonjwa akilini hivyo anahitaji ushauri wa kisaikolojia.
“Huyo Aunt Ezekiel anahitaji ushauri nasaha kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa watu wengine wenye tatizo kama lake. Anapaswa kusikiliza maelekezo ya Basata kwamba nguo zisizo na maadili ya Mtanzania hazitakiwi katika sanaa yetu, aache mara moja.
“Kila Jumatatu huwa tuna Jukwaa la Sanaa hivyo tumeshakutana na wasanii hao na kuwaeleza tatizo hilo lakini wamekuwa wagumu wa kuelewa. Tumeona njia pekee ya kuwasaidia ni kuwapa ushauri wa bure juu ya madhara ya kuvaa nguo hizo,” alisema mkurugenzi huyo kwa staili ya kumpa onyo kali msanii huyo.
Hivi karibuni, Aunt akiwa kwenye ziara ya Tamasha la Serengeti Fiesta 2012 mkoani Mwanza alijikuta akilewa na kushindwa kujisitiri kutokana na kigauni alichokuwa amevaa kilichoacha wazi sehemu kubwa ya maumbile yake muhimu.