Na Mwandishi Wetu
MIKAKATI na kampeni za majitaka zenye lengo la kumchafua Mbunge wa Jimbo la Busega mkoani Simiyu, Dk. Titus Kamani, zimeanza kubainika kwa kumhusisha tena na tuhuma za mauaji.
Dk. Kamani, ambaye ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa mpya wa Simiyu, ameanza kuchafuliwa akihusishwa na tuhuma za kutaka kumuua aliyekuwa mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, aliwahi kueleza bayana kuwa wamefanya uchunguzi wa kina na kubaini Dk. Kamani hahusiki na tuhuma hizo na kwamba, waliotuhumiwa wameshafikishwa mahakamani.


“Hatumtafuti Dk Kamani, tukimhitaji tutampata lakini katika uchunguzi wetu tumebaini tuhuma hizo hazimuhusu," alikaririwa Kamanda Barlow baada ya kuibuka kwa uvumi kuwa mbunge huyo alikuwa akisakwa na polisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam, jana, Dk. Kamani amesema kumekuwepo na kampeni chafu za kuhakikisha jina lake linachafuka ili kudhoofisha harakati zake za kukitumikia Chama.
Amesema kuwa tangu alipojitosa kuwania nafasi hiyo, kumekuwepo na mikakati ya kumchafua inayofanywa na baadhi ya wanasiasa wakiwemo waliopo ndani ya CCM na kwamba, hilo amelibaini na atalifikisha kwenye vikao husika.
Dk. Kamani katika taarifa yake amesema kuwa, mbinu chafu hizo zimekuwa zikisukwa na wanasiasa hao kwa lengo la kumchafua na kumchonganisha na wapigakura wake pamoja na jamii imuone kuwa hafai.
“Makovu na visasi vya kushindwa katika uchaguzi uliopita kamwe havitaiharibu Busega wala kunidhoofisha kuwatumia wananchi wangu. Nafahamu hizi ni mbinu chafu kwa ajili ya kuniharibia katika harakati zangu za kuwania nafasi ndani ya Chama," alisema katika taarifa hiyo.
Tayari watu wanaotuhumiwa kuhusika katika njama za kutaka kumuua Dk. Chegeni wameshapandishwa kizimbani kujibu mashitaka hayo.