Jaji Mkuu wa Tanzania, akiwapa nasaha Mahakimu wapya mara
baada ya kuwaapisha Mahakimu hao (angalia chini ) hivi katika Chuo cha
Uongozi wa Mahakama (IJA) kilichopo Lushoto-Tanga.
Picha na mdau Mary Gwera wa Mahakama
)


 
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman
amewaapisha na kuwaasa juu ya utendaji kazi Mahakimu Wakazi wa Mahakama za
Mwanzo walioajiriwa hivi karibuni.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Mahakimu 372 katika hafla iliyofanyika katika Chuo cha
Uongozi wa Mahakama (IJA) wilayani Lushoto hivi karibu, Mhe. Chande alisema
kuwa Mahakimu hao watumie fursa waliyoipata katika kutoa haki sawa na kwa
wakati stahiki.

“Mahakama imejiwekea mkakati wa kuajiri Mahakimu wenye
shahada ya Sheria, na kwa mara ya kwanza tumefanikiwa kuajiri jumla ya Mahakimu
300 wenye shahada ya sheria, hivyo, Mahakama na jamii kwa ujumla ina matumaini
makubwa juu ya ujio wenu katika suala zima la utoaji haki,” alibainisha Jaji
Mkuu.

Alisema kuwa asilimia 70 ya mashauri yapo katika
Mahakama za Mwanzo jambo ambalo linapelekea wingi la mashauri na hivyo kuwataka
Mahakimu kusikiliza na kuzitolea maamuzi kwa wakati kesi ambazo ushahidi tayari
wake umekamilika.

Aliongeza kwa kutaja sifa za Hakimu bora na kuainisha
kuwa anatakiwa kuwa anayetoa maamuzi kwa kuzingatia haki, sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa.

“Hakimu bora anatakiwa pia kulinda heshima ya Mahakama
na taaluma yake na ya Mahakimu wenzake,
pamoja na kuheshimu wajibu wake kwenye jamii husika na vilevile kufuata maadili
ya kazi katika suala la utoaji haki,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi, Mhe. Fakih Jundu
aliwaasa pia Mahakimu hao kuzingatia haki za washitakiwa ikiwemo upatikanaji wa
dhamana endapo mshitakiwa husika anastahili.

“Ni muhimu kwenu kuzingatia haki za washitakiwa na
kuepuka matumizi mabaya ya vifungu vya sheria, mkifanya hivyo mtajiweka katika
nafasi nzuri ya kufanya maamuzi ambayo
hayakiuki misingi ya haki,” alisema Jaji Kiongozi.

Sambasamba ya shughuli ya kuwaapisha Mahakimu hao, pia
wamepata mafunzo ya wiki moja kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Mahakama juu ya
utendaji kazi wa kila siku hususani suala zima la utoaji haki nchini.

Jumla ya Mahakimu 372 wameapishwa na Mhe. Jaji Mkuu, kuwa
Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo zilizoko katika vituo mbalimbali nchini,
Mahakimu 72 ambao walikuwa tayari kazini wameapishwa pia kuwa Mahakimu Wakazi
baada ya kupata Shahada ya Sheria.