Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni Tanzania Profesa Hermas Mwansoko akitoa maelekezo kwa wajumbe wa Jumuiya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki  
Kamishna wa Utamaduni Zanzibar Hamad Bakar Mshindo (kulia) akitoa maelezo ya Jengo hilo ambalo ndio Makao makuu ya Jumuiya ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.
Picha ya pamoja ya wajumbe wa Jumuiya ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki katika Makao Makuu Zanzibar.
 
Na Miza Kona.
Kuwepo kwa Makao makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini Zanzibar kutasaidia kukuza Lugha ya Kiswahili, Utamaduni na Michezo kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni Tanzania Profesa Hermas Mwansoko amesema hayo wakati walipokuwa wakijadili uanzishwaji wa Makao makuu ya kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuangalia Itifaki ya kuanzisha Kamisheni ya Utamaduni na Michezo.
Amesema kuwa Zanzibar ni chimbuko la Kiswahili sanifu hivyo ni vyema kuirejesha historia ya kiswahili hapa nchini ili kiweze kukuwa zaidi na kuwepo muendelezo mzuri wa lugha, utamaduni na michezo kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Aidha Profesa Mwansoko amesema kuanzishwa kwa jumuiya hiyo Zanzibar kutatoa nafasi za ajira kwa wazanzibari wenyewe kwani wataweza kupata ajira na kuweza kutoa wataalamu wazuri wa lugha ya Kiswahili jambo ambalo litapelekea maendeleo nchini.
Amefahamisha kuwa, kuwepo kwa makao makuu hayo hapa nchini kutaweza kudumisha mashirikano ya karibu kwa wanachama wa Afrika Mashariki katika mambo ya utamaduni na michezo.
Kwa upande wao washiriki wa Mkutano huo wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wao na kuweza kukubali Makao makuu ya Kamisheni hiyo kuwepo Zanzibar na kutoa fursa nzuri ya kukikuza kiswahi katika nchi za Afrika ya Mashariki.