Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea nakala ya machapisho mbalimbali ya Bunge la Afrika Mashariki toka kwa Spika wa Bunge hilo Bi. Margaret Banbtonbg Zziwa alipomtembelea Ikulu Jumatano Septemba 19, 2012.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIRais Jakaya Mrisho Kikwete amelishauri Bunge la Afrika Mashariki (EAC) kuzingatia na kufuata maelekezo yaliyomo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo wakati wa kuwasilisha na kujadili hoja zao.
Rais Kikwete ametoa ushauri huo jana jioni (19 Septemba, 2012) alipokutana na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mheshimiwa Margareth Ziwa, Ikulu.
“Jumuiya ya Afrika Mashariki inahusika na masulala yaliyomo kwenye Mkataba (Treaty) na Itifaki zilizoanzisha Jumuiya hii na kila nchi inawajibu wa kuzingatia kilichomo kwenye Mkataba” ameeleza na kufafanua “Lakini pia msisahau kuwa hizi ni nchi huru zenye sheria na taratibu zake ambazo nchi zinapaswa kuzifuata na kuzizingatia, hivyo Bunge la Afrika Mashariki linaweza tu kuzishauri lakini sio kuzielekeza au kuzilazimisha kutekeleza jambo ambalo halimo kwenye Mkataba ambao nchi hizi zimetiliana saini” ameongeza.
Mheshimiwa Ziwa amefika Ikulu kujitambulisha kwa Mheshimiwa Rais baada ya kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Mheshimiwa Ziwa ni raia wa Uganda na ni Mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inajumuisha nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania.
Rais amewataka wabunge wapya kusoma Mkataba na Itifaki zilizoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri bila kuingilia uhuru na taratibu za nchi wanachama.
“Jipeni muda wa kutosha wa kusoma na kuzielewa taratibu za Mkataba na Itifaki iliyoanzisha Jumuiya hii, hii itawasaidia sana katika kujenga hoja zenu na jinsi ya kuziwasilisha” amewakumbusha kuwa hiyo ndiyo njia pekee ambayo itawafanya kutekeleza kazi na wajibu wao kwa umakini na uangalifu bila kuingilia taratibu za mabunge ya nchi wanachama.
Wakati huo huo, leo asubuhi (20 Septemba, 2012) Rais amekutana na Katibu Mkuu wa EAC Dkt. Richard Sezibera ambaye amefika kumueleza Rais juu ya maendeleo na ratiba ya shughuli muhimu za Jumuiya hiyo ambazo EAC inatarajia kuzifanya kabla ya mwisho wa Mwaka.
Rais amempongeza Dkt. Sezibera kwa maendeleo ya Jumuiya hiyo na jinsi shughuli za utekelezaji zinavyokwenda kulingana na ratiba ya EAC.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu.
Dar-Es-Salaam
20 Septemba, 2012